Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 22:13

Wanajeshi wa Kenya wamewasili DRC huku waasi wakikaribia Goma


Wanajeshi wa Kenya baada ya kuwasili mjini Goma, DRC kupambana na makundi ya waasi Nov 12, 2022
Wanajeshi wa Kenya baada ya kuwasili mjini Goma, DRC kupambana na makundi ya waasi Nov 12, 2022

Wanajeshi wa Kenya wamewasili Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa ajili ya kupambana na makundi ya waasi ambayo yamesababisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo kwa miongo kadhaa.

Wanajeshi 903 wa Kenya wameingia DRC chini ya makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wanajeshi hao watashika doria katika mji wa Goma, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako mapigano makali yameripotiwa Ijumaa, kati ya wanajeshi wa serikali ya DRC na kundi la waasi la M23.

Kamanda wa kikosi cha Kenya Luteni Kanali Dennis Obiero, ameambia waandishi wa habari mjini Goma kwamba lengo lao kubwa ni “kumshambulia adui kwa ushirikiano na jeshi la DRC na kusaidia katika kuyapokonya silaha makundi ya waasi.”

Obiero amesema kwamba “ukosefu wa usalama ni jambo ambalo linaharibu maisha ya kila mtu katika jamii.”

Ameeleza kwamba jeshi la Kenya litashirikiana na mashirika ya kutoa misaada katika kurejesha utulivu na amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kuna zaidi ya makundi ya waasi 120 mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, ambayo yamekuwa yakishambulia raia, kusababisha vifo na uharibifu wa mali.

Waasi wa M23 wameongeza mashambulizi

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea kati ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika sehemu ya Rugari, Kivu Kaskazini tangu Ijumaa.

Kulingana na mwandishi wa VOA mjini Goma, mapigano kati ya waasi hao na wanajeshi wa DRC yanaendelea katika mji wa Kibumba, kilomita 25 kutoka Goma.

Mji wa Goma ni mji mkubwa wa kibiashara, wenye zaidi ya watu milioni moja.

Usambazaji wa nguvu za umeme umetatizika mjini Goma ambapo waasi hao wanalenga kudhibiti.

Kundi la M23 liliwahi kudhibiti mji wa Goma mnamo mwaka 2012 kabla ya kufurushwa na jeshi la serikali.

Kundi hilo limedhibiti mji wa Bunagana, mpakani na Uganda.

Wanajeshi wa Kenya baada ya kuwasili Goma, DRC Nov 12 2022
Wanajeshi wa Kenya baada ya kuwasili Goma, DRC Nov 12 2022

Mgogoro kati ya DRC na Rwanda

Serikali ya DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Rwanda imekanusha.

Rais wa Kenya William Ruto ameitaja hatua ya kutuma jeshi la Kenya nchini DRC kuwa muhimu sana na swala la dharura.

Jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki litajumulisha pia wanajeshi kutoka Uganda, Burundi na Sudan Kusini.

Kikosi hicho kitakuwa chini ya kamanda wa Kenya.

DRC imekataa wanajeshi wa Rwanda wasiwe sehemu ya kikosi hicho cha jeshi.

DRC imemfukuza balozi wa Rwanda mjini Kinshasa mwezi uliopita na kumuita balozi wake wa mjini Kigali kurudi Kinshasa.

Rais wa Angola Joao Lourenco amekuwa Rwanda anatarajiwa nchini DRC leo Jumamosi kwa mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Rwanda na DRC na namna ya kumaliza mapigano huku rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akitarajiwa kuwasili jumapili.

Mwandishi wetu wa Goma, Austere Malivika amechangia ripoti hii.

XS
SM
MD
LG