Maelfu ya wakenya waliandamana mjini Nairobi Jumamosi wakidai hatua mbadala zichukuliwe kuwalinda wanyamapori na kusitisha biashara ya pembe za ndovu na wanyama wengine.
Kwa mujibu wa waziri wa utalii nchini Kenya, Najib Balala maandamano yaliandaliwa ili kufanyia kampeni pendekezo ambalo Kenya inalengo la kuliwasilisha wakati wa mkutano ujao wa biashara ya kimataifa ya wanyama walio hatarini utakaofanyika Sri Lanka mwezi Mei. Akizungumza wakati wa maandamano hayo Balala alieleza kwamba vipaumbele vya juu kwenye mkutano huo vitakuwa kutafuta hatma ya kusitisha biashara ya pembe za ndovu na kudhibiti biashara za mnyama aina ya Twiga.
Nchi kadhaa za Afrika na baadhi zenye idadi kubwa sana ya tembo, mwanzoni mwa mwaka huu zilishinikiza kulegeza vizingiti katika biashara halali ya pembe za ndovu, wakati kundi jingine la nchi za Afrika zinahimiza kuwepo na udhibiti zaidi ikiwa ndio njia bora ya kusitisha uuaji haramu wa tembo kwa ajili ya kuchukua pembe zao.