Hatua hiyo ni kufuatia kusitishwa kwa misaada ya kigeni ya Marekani kwa siku 90 ambako kulitangazwa na rais wa Marekani Donald Trump muda mfupi baada ya kuapishwa Januari 20. Serikali ya Malawi inajitahidi kuhakikisha kwamba wanafunzi hao wanaendelea na masomo yao, lakini vyuo vimeonya kuwa haviwezi kumudu gharama yao bila usaidizi.
Serikali ya Marekani kupitia shirika la Kimataifa la Maendeleo USAID, kwa muda mrefu imekuwa ikifadhili masomo ya maelfu ya wanafunzi kwenye vyuo vya umma vya Malawi, na sass hatua hiyo imeathiri vyuo vingi kikiwemo kile cha Kilimo na Mali Asilia cha Lilongwe, kile cha Afya na Sayansi cha Kamuzi pamoja na kile cha Sayansi na Teknolojia cha Malawi, MUST.
Patience Yamikani Chakwama mwanafunzi anayefadhiliwa na USAID kwenye chuo kikuu cha MUST, ameambia VOA kwamba tayari ameathirika. Yeye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na amesema kuwa kusitishwa kwa misaada ya kigeni kulitangazwa kabla ya wanafunzi kupokea fedha za matumizi ya kila siku.
Chakwama amesema kuwa kando la kulipiwa ada ya shule pamoja na makazi, USAID pia ilikuwa ikitoa fedha za chakula na huduma za internet kwenye simu zao. Utawala wa Trump unasema kuwa ulichukua hatua ya kusitisha msaada huo kwa siku 90 ili kuhakikisha kuwa fedha za USAID zinatumika kulingana na sera na maslahi ya Marekani. Sitisho hilo litaendelea hadi Aprili 20.
Forum