Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 10:42

Wanafunzi kutoka Afrika Mashariki ni kati ya walengwa wa masharti makali ya viza kuingia Marekani


Viza ya Marekani
Viza ya Marekani

Serikali ya Marekani ina mipango ya kuwadhibiti wanafunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki na kwingineko duniani, kwendelea na masomo kwenye vyuo vikuu nchini humo, kwa kuweka masharti mapya ya viza, ambayo yatadhibiti ukazi wao.

Aidha, iwapo mapendekezo ya hivi karibuni ya wizara ya usalama wa ndani ya Marekani yatatekelezwa, wanafunzi kutoka nchi nyingi za Afrika, zikiwemo Kenya, Tanzania na Uganda, watazuiliwa kupata viza za kukaa nchini kwa Zaidi ya miaka miwili.

Hii ina maana kwamba wanafunzi hao wa kigeni ambao watakuwa na nia ya kuhitimu kwa shahada zinazochukua Zaidi ya miaka miwili katika vyuo vikuu vya Marekani, hawataweza kufanya hivyo.

Kulingana na utawala wa Rais Donald Trump, mapendekezo hayo yanalenga nchi ambazo zimerekodi Zaidi ya asili mia kumi ya wanafunzi ambao wamezidisha muda wao wa kuwa nchini, kinyume na masharti ya viza zao.

Wanafunzi watakaoathiriwa moja kwa moja iwapo hatua hiyo itachukuliwa ni wa kutoka Kenya, Rwanda, Uganda, Tanzania, Burundi, South Sudan, Somalia, and Ethiopia, Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Central African Republic, Chad, DR Congo, Republic of Congo, Côte d'Ivoire, Djibouti, Equatorial Guinea, Eritrea, Gabon, the Gambia, Ghana, Guinea, Guinea-Bissau, Liberia, Libya, Malawi, Mali, Mauritania, Niger, Nigeria, North Korea, Papua New Guinea, Senegal, Sierra Leone, Sudan, Togo na Zambia.

Wengine ni kutoka Afghanistan, Bhutan, Guyana, Haiti, Iran, Iraq, Kosovo, Kyrgyzstan, Moldova, Mongolia, Nepal, North Korea, Papua New Guinea, Philippines, Samoa, Syria, Tajikistan, Tonga, Turkmenistan, Tuvalu, Uzbekistan, Vietnam na Yemen.

Kenya inaorodheshwa nambari moja kati ya nchi za Afrika Mashariki zilizo na wanafunzi wengi kwenye vyuo vikuu vya Marekani na ni ya tatu kati ya nchi za bara za Afrika zilizo mashariki mwa jangwa la Sahara kwa idadi kubwa ya wanafunzi hao, ikifuatiwa na Ethiopia.

Nigeria, ambayo inaongoza kwenye orodha hiyo, ilikuwa imewatuma wanafunzi 13,423 mwaka jana, ambalo ni ongezeko la takriban asili mia sita kutoka kwa kipindi cha kati ya mwaka wa 2017 na 2018. Ya pili kwa wingi wa wanafunzi ni Ghana.

Ingawa wizara hiyo inasema kuna uwezekano kwa wanafunzi kuomba waongezewe muda wa viza zao baada ya miaka hiyo miwili, hakuna hakikisho kwamba wataongezewa muda huo.

Wakili wa masuala ya uhamiaji Aaaron Reinchlin-Melnick, ambaye pia ni mchambuzi wa sera za uhamiaji katika baraza la Uhamiaji wa Marekani, amenukuliwa na gazeti la The East African akisema kwamba hatua hiyo itawaathiri wanafunzi wengi na kusababisha wasiwasi kuhusu mstakabal wa elimu yao.

“Iwapo mapendekezo hayo ya Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani yatatekelezwa, wanafunzi wa kigeni kutoka nchi kama Kenya, Nigeria, Vietnam na Ufilipino hawataweza kupata shahada zao katika vyuo vinavyotoa mafunzo ya miaka minne,” alisema wakili Reinchhlin-Melnick.

Mapendekeo hayo pia yanazitaka viza za ukazi wa wanafunzi kutoka kwa nchi ambazo zimeorodheshwa kama wadhamini wa ugaidi (Sudan, Iran, Syria na Korea Kaskazini), kuwa za miaka miwili pekee.

Wachambuzi hata hivyo wanaeleza kwamba iwapo vigezo viunavyotumiwa vianazingatia nchi zilizo na watu wengi waliozidisha muda wao wa ukazi nchini Marekani, basi nchi kama China, India, Brazil na Canada, ndizo zingeongoza kwenye orodha hiyo kwa sababu zina idadi kubwa Zaidi ya raia waliozidisha muda wao wa ukazi.

Kwa jumla, idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaoingia Marekani imepungua, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani kwa ushirikiano na taasisi ya elimu ya kimataifa mijini New York.

Moja ya sababu zilizotolewa, kulingana na utafiti huo, ni kwamba wazazi wanaogopa kuwapeleka watoto wao Marekani hususan kufuatia ongezeko la ghasia na visa vya mashambulizi ya bunduki dhidi ya Wamarekani weusi.

Mapema mwaka huu, serikali ya Marekani ilifutilia mbali mipango yake ya kuwarudisha makwao wanafunzi wa kigeni ambao masomo yao yanafanyika tu kupitia mitandao kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Uamuzi huo wa utawala wa Trump ulijiri wiki moja baada ya kutangazwa kwa sera hiyo. Taasisi ya technolojia ya Masachussets (MIT) na chuo kikuu cha Havard viliishtaki serikali kufuatia mpango huo.

Jaji wa wilaya Allison Burroughs mjini Masachussets alisema kwamba pande zote mbili zilikuwa zimeafikiana.

XS
SM
MD
LG