Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:15

Wanafunzi ni miongoni mwa waliotekwa Nigeria


Wakiandamana na wanajeshi ni wasichana wa shule ya Chibok waliotekwa nyara, Hauwa Joseph (kushoto) na Mary Dauda (kulia) wakiwa wamebeba watoto wao walipowasili katika kambi ya Maimalari huko Maiduguri, kaskazini-mashariki mwa Nigeria, Juni 21, 2022. Picha na Audu MARTE / AFP.
Wakiandamana na wanajeshi ni wasichana wa shule ya Chibok waliotekwa nyara, Hauwa Joseph (kushoto) na Mary Dauda (kulia) wakiwa wamebeba watoto wao walipowasili katika kambi ya Maimalari huko Maiduguri, kaskazini-mashariki mwa Nigeria, Juni 21, 2022. Picha na Audu MARTE / AFP.

Wanafunzi kumi wametekwa nyara kaskazini magharibi mwa Nigeria katika jimbo la Kaduna ambako magenge ya wahalifu awali yaliwateka watoto kadhaa, afisa wa serikali alisema Jumanne.

Waathirika ambao ni wanafunzi wa shule ya sekondari ya Awon katika wilaya ya kati ya Kachia walikamatwa Jumatatu katika mazingira yasiyoeleweka, alisema Samuel Aruwan kamishna wa maswala ya ndani na usalama wa jimbo la Kaduna.

Bado haiko wazi kama wanafunzi hao walitekwa nyara kutoka kwenye eneo la shule au wakati wanakwenda shule, ambapo shule hiyo ni ya kutwa.

Wakati huo huo, watu takriban 12 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa au kutekwa nyara katika mfululizo wa mashambulizi katika meneo ya kaskazini mashariki na katikati mwa Nigeria, polisi na maafisa wa serikali walisema Jumatatu.

Siku ya Jumatatu huko kaskazini mashariki katika Jimbo la Adamawa, watu wasiojulikana wakiwa na silaha walivamia kijiji cha Dabna kilichopo wilaya ya Hong, na kusababisha "mauaji ya kusikitisha ya watu watatu", msemaji wa polisi wa eneo hilo Suleiman Nguroje alisema, na kuongeza kuwa katika tukio hilo pia nyumba ziliteketezwa moto.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo ingawa wanajihadi wa Boko Haram wanajulikana kufanya mashambulizi katika eneo hilo kuanzia eneo la msitu wa Sambisa uliopo jirani na jimbo la Borno.

Pia siku ya Jumatatu, watu wenye silaha walishambulia vitongoji vilivyopo katika eneo la Oganenigu kwenye wilaya ya Dekina katika jimbo la kati la Kogi, kulingana na mamlaka ya eneo hilo.

Msemaji wa gavana Muhammed Onogwu alisema kuwa mwanasiasa wa eneo hilo aliuawa wakati wengine "waliathiriwa na shambulio hili baya na la kusikitisha".

Siku ya Jumapili, watu wenye silaha walivamia kanisa katika kijiji cha Akenawe-Tswarev kilichopo Jimbo katikati la Benue, na kumuua muumini mmoja na kuwateka nyara watu wengine watatu, kulingana na Salome Tor, ambaye ni msimamizi wa masuala ya kisiasa katika wilaya ya Logo, eneo ambalo kijiji hicho kilipo.

"Wakati wa ibada ya asubuhi, watu hao wenye silaha walivamia kanisa na kumpiga risasi mtu mmoja na kuwateka nyara watu wengine watatu, akiwemo kasisi," Tor alisema.

Waumini wengine wawili walijeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitali kwa matibabu, alisema.

Katika Jimbola kati la Niger siku ya Jumamosi, watu wenye silaha wanaoshukiwa kutoka magenge ya kihalifu walivamia vijiji kadhaa katika wilaya za Mashegu na Munya, na kuua takriban watu saba na kuwateka nyara wengine 26 kulingana na afisa wa eneo hilo.

Polisi katika Jimbo la Niger hawakujibu ombi la shirika la habari la AFP la kuwataka kutoa maoni yao kuhusu mashambulizi hayo na utekaji nyara.

Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la Reuters.

XS
SM
MD
LG