Wamarekani wanaadhimisha miaka 242 tangu kujitenga na utawala wa Uingereza kwa utaratibu wa kawaida wa siku nzima inayo sheherekewa kwa vyakula, maandamano na fataki nchi nzima.
Rais wa Marekani Donald Trump na mkewe Melania watafanya karamu kwa kuzikirimu familia za wanajeshi huko White House.
Sikukuu ya Julai 4 ina utamaduni wa kusoma Tamko la Uhuru katika ngazi za jengo la Kumbukumbu la Taifa mjini Washington.
Ndani ya jengo, waraka wa awali umetundikwa na kuweza kuonekana na kila mtu pamoja na Katiba na Muswada wa Haki za binadamu kwa ajili ya umma wa Marekani kuweza kuuona.
Muda mfupi baada ya kusomwa tamko hilo, matembezi yaliyo hudhuriwa na maelfu ya watu huanza mbele ya jengo hilo katika barabara ya Constitution na matembezi hayo yanapita mitaa kumi kuelekea magharibi ya mji wa Washington, na kumalizika mara baada ya kupita kati ya jengo la White House na kumbukumbu ya rais wa kwanza wa Marekani, George Washington.
Washington D.C. pia itakuwa na maonyesho kwenye Bunge la Marekani wakati vikundi vya Beach Boys, Chita Rivera, Andy Grammer, The Temptations, CeCe Winans na bendi ya Symphony Orchestra ya taifa, pamoja na vikundi vingine vitakapo watumbuiza wananchi.
Sherehe hizo humalizika na maonyesho ya fataki baada ya jua kuzama.