Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 03, 2025 Local time: 04:09

Wakuu wa nchi na serikali za Kiafrika wakutana Nairobi kujadili masuala ya AU


Rais wa Kenya William Ruto aliyekuwa mwenyeji wa viongozi wa AU mjini Nairobi Jumatatu.
Rais wa Kenya William Ruto aliyekuwa mwenyeji wa viongozi wa AU mjini Nairobi Jumatatu.

Wakuu wa Nchi na serikali 5 za Afrika wamekutana jijini Nairobi Jumatatu kujadilia  marekebisho ya kitaasisi ya Umoja wa Afrika, AU, na kukubaliana kuhusu haja ya kuharakisha mageuzi ya kuwezesha AU kutekeleza vipaumbele vyake bila kutegemea fedha za kigeni.

Marais William Ruto wa Kenya, Azali Assoumani wa Comoro, Umaro Sissoco Embaló wa Guinea-Bissau, John Dramani Mahama wa Ghana, na Taye Atske Selassie wa Ethiopia, na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, wakati wa kikao hicho wamekubaliana kuhusu haja ya kuharakisha mageuzi ya kuwezesha AU kutekeleza vipaumbele vyake, "bila kutegemea vyanzo vya nje vya kifedha kuiwezesha kufadhili bajeti, shughuli na programu zake kwa uendelevu wa kutabirika, usawa na uwajibikaji, kwa ukamilifu na kwa kutegemea nchi zote wanachama", Ruto ameeleza.

Viongozi hao wameeleza kuwa AU, lazima ifanyiwe marekebisho yanayohitajika kuwezesha ufanisi zaidi unaendana na uhuru wa kifedha na ufaao kwa madhumuni ili kuzingatia zaidi mahitaji ya sasa na ya siku za usoni barani Afrika. Ili kufikia malengo ya mabadiliko ya kudumu na yenye matokeo chanya, viongozi hao wameeleza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika na Kamisheni hiyo, Baraza la marais na Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu kutekeleza kwa kasi yanayokubaliwa, kwa usahihi na ufanisi.

Ruto anaongoza mkutano huo kwa nafasi yake kama bingwa wa mageuzi ya kitaasisi katika Umoja wa Afrika, jukumu alilotwikwa mwaka 2024 kutoka kwa rais wa Rwanda Paul Kagame. Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, ameeleza kuwa mageuzi ya Umoja wa Afrika yanahitajika kwa sasa kutokana na vipaumbele vinavyobadilika na nafasi hii ni fursa muhimu kwa Afrika kufikia malengo yake.

Marekebisho yanayotajwa na Ruto ni yale yanayolenga kuhuisha muundo, utendakazi na mwelekeo wa Tume ya Umoja wa Afrika, mihimili ya AU, na mashirika maalumu ili kuyafanya kuwa na ufanisi katika kusimamia mipango ya AU pamoja na kuharakisha utekelezaji wa Mkataba unaoanzisha Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Marekebisho hayo pia yanajumuisha kuimarisha uhuru wa kifedha, kupunguza utegemezi wa wafadhili kutoka nje na kuhakikisha uhuru wa kifedha wa umoja huo. Ruto atawasilisha ripoti ya mwisho kuhusu mapendekezo ya mageuzi hayo wakati wa Kikao cha 38 cha Kawaida cha Baraza Kuu la marais wa AU, kilichopangwa kufanyika Februari, tarehe15-16, Addis Ababa, Ethiopia.

KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.

Forum

XS
SM
MD
LG