Wahusika wakuu ndani na kuzunguka Syria wameanza kuyaweka sawa majeshi yao wakati majadiliano yanaendelea jinsi ya kusonga mbele mara majeshi ya Marekani yakapoondoka nchini humo na mapambano dhidi ya mabaki ya kundi la kigaidi la Islamic State ambalo limejitangazia ukhalifa.
Kasi ya harakati za wanajeshi pamoja na mawasiliano ya kidiplomasia, yaliongezeka Jumatatu siku ambayo Pentagon imethibitisha kuwa waziri wa ulinzi anayeondoka madarakani Jim Mattis ameamuru wanajeshi wa Marekani kuanza kuondoka Syria bila ya kufafanua.
Amri ya kiutendaji kwa Syria imetiwa saini afisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani ameithibitisha kwa Sauti ya Amerika-VOA na kuongezea "sitaweza kutoa maelezo zaidi ya operesheni kwa wakati huu".
Rais Donald Trump alituma ujumbe wa Twitter siku ya Jumapili kwamba yeye na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan walizungumza kwa simu na kwamba kuondoka kwa Marekani kutakuwa kwa kasi ya pole pole na kwa uratibu wa hali ya juu. Msemaji wa Erdogan alisema Jumatatu kuwa maafisa wa ulinzi wa Uturuki watakutana na wenzao wa Marekani wiki hii.