Maelfu ya watu walikusanyika Jumapili kwenye tamasha huko Johannesburg la kuenzi maisha ya Nelson Mandela nchini Afrika kusini.
Tamasha hilo la maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Rais wa kwanza mweusi huko Afrika kusini Nelson Mandela liliandaliwa na kundi la wanaharakati la Global Citizen na mwanamuziki kutoka Marekani Beyonce Knowles aliongoza waimbaji nyota wengine waliokuwepo ndani ya tamasha hilo. Pia tamasha hilo lililenga kuelezea mapambano dhidi ya umaskini, ukosefu wa usawa wa kijinsia na njaa ambayo Nelson Mandela aliyapigania.
Rais wa Benki ya Dunia Jim Kim alikuwa miongoni mwa viongozi wa kisiasa na biashara waliohudhuria tamasha hilo na alitangaza dola bilioni 1 za uwekezaji katika afya na elimu kote barani Afrika katika mwaka 2019.
Wakati huo huo, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alionekana kupitia video na aliahidi kuongeza bajeti ya elimu nchini kwake kufikia asilimia 30 ya bajeti jumla.
Richard Branson pia alionekana kupitia video alitangaza dola milioni 105 kutoka kwa wafadhili wakiwemo UK Aid, Virgin Unite na Bill and Melinda gates Foundation kuelekea kumaliza ugonjwa wa macho unaojulikana kitaalam Trachoma ambao unasababisha upofu.
Baadhi ya wanamuziki maarufu waliohudhuria na kuimba kwenye tamasha la Global Citizen lililofanyika kwenye uwanja wa mpira wa FNB mjini Johannesburg ni Jay Z, Usher na Ed Sheeran.