Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:03

Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wamewafukuza waasi wa M23 Rubaya


Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, FARDC, wakiwa katika mji wa Sake kupambana na waasi wa M23.
Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, FARDC, wakiwa katika mji wa Sake kupambana na waasi wa M23.

Waasi kutoka muungano wa makundi yanayolisaidia jeshi la serikali ya DRC wanaripoti kwamba wamewashinda nguvu na kuwafukuza waasi wa kundi la M23 kutoka Rubaya, baada ya kuudhibithi mji huo kwa muda mfupi.

Jean Mulumba, msemaji wa kundi la waasi la Wazalendo, ameiambia Sauti ya Amerika VOA, kwamba mapigano makali katika mji huo yamepelekea waasi wa M23 kuondoka.

Mulumba vile vile amesema kwamba muungano wa Wazalendo umewafukuza waasi wa M23 kutoka Bihabwe, akiongezea kwamba “vita haviwezi kukosa vifo na majeruhi.”

Amesema kwamba “mapigano yanaendelea Mweso ambapo waasi wa M23 wanaudhibithi kwa sasa, akilishutumu jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa “kutofanya vya kutosha kulisaidia jeshi la DRC kupambana na makundi ya waasi yanayopigana na serikali.”

Amedai kwamba “sehemu ambazo zinashikiliwa na wanajeshi wa EAC ndio zinazotumiwa na waasi wa M23 kuingia kutoka Rwanda. Hao siyo waasi wa M23 hao ni wanajeshi wa Rwanda. Wanaingia wakiwa na silaha mpya na za kisasa, wana sare mpya. Tunajua sare zao.” VOA haijaweza kuthibitisha madai hayo. Juhudi za VOA kumfikia msemaji wa kundi la M23 hazijafanikiwa.

Mapigano yamekuwa yakiongezeka mashariki mwa DRC licha ya masharti ya wapatanishi

Mapigano makali yanaendelea Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya jeshi la serikali FARDC na waasi wa kundi la M23.

Waasi wa M23 waliuteka mji wenye shughuli za uchimbaji madini wa Rubaya, ulio magharibi mwa Sake na Goma.

Kulingana na ripoti ya shirika linalofuatilia mapigano ya DRC, Crisis 24, waasi wa M23 vile vile wanadhibiti miji ya Kingi na Karuba.

Waasi wa M23 waliuteka mji wa Mushaki mnamo Februari 24.

Mamia ya watu wamelazimika kuhama sehemu ambazo waasi hao wanazishikilia.

Sehemu ambazo wamezidhibiti zipo kwenye barabara kati ya Masisi na Goma, inayotumika kwa usafiri wa bidhaa kuingia Goma.

Waasi hao walichukua udhibiti wa Kitchanga Januari 26.

Mapigano yanaendelea Mweso na Kitchanga na kuzuia ufanisi wa waasi kuingia Goma.

Waasi wa M23 walitakiwa kuondoka sehemu ambazo wanazishikilia kulingana na makubaliano wa viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Waasi wa M23 wameongeza mashambulizi tangu mwezi Novemba 2021, wakilenga kambi za jeshi za serikali, mashariki mwa DRC.

Amri ya kuacha mapigano

Mapigano hayo yamepeleka mgogoro wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. DRC inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23. Rwanda inakanusha madai hayo licha ya ripoti kadhaa ikiwemo ya wataalam wa Umoja wa Mataifa kuitaka Rwanda kuacha kuwaunga mkono waasi wa M23. Marekani vile vile imeitaka Rwanda kuacha kuwaunga mkono waasi wa M23.

Mnamo Juni 2022, waasi wa M23 walidhibiti mji wa Bunagana na kuanza kupigana wakielekea Goma na wameteka sehemu kadhaa kwenye njia kuu ya kuelekea Goma.

Waasi wa M23 wanalenga kuilazimisha serikali ya Kinshasa kukubali makubaliano ya amani ya mwaka 2013, wakiwataka wapiganaji wake kujumuishwa katika jeshi la taifa, miongoni mwa mambo mengine.

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekuwa wakiimarisha juhudi za kutaka vita hivyo kumalizika, tangu Novemba 2022 lakini waasi wa M23 wameendelea kutekeleza mashambulizi.

Kundi hilo limekuwa likitaka kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya DRC ambayo imesema kwamba haiwezi kufanya maungumzo na ‘magaidi’.

XS
SM
MD
LG