Maelfu ya wakimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wameingia kusini magharibi mwa Uganda katika wilaya ya Kisoro wakitoroka mapigano mapya yanayoongozwa na kundi la M23 nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Vyombo vya habari vya Uganda vinaripoti kwamba Jeshi la Uganda UPDF limeimarisha doria mpakani mwa Uganda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo baada ya kutokea mapigano makali Bunagana, kivu kaskazini, kilomita 5 kutoka mpaka wa Uganda na DRC.
Kulingana na mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika VOA, mjini Goma, Austere Malivika, kambi 5 za jeshi la DRC zimetekwa na wapiganaji wa M23 kufikia sasa, japo jeshi la DRC limeimarisha mashambulizi dhidi ya waasi hao kujaribu kurejesha udhibithi wa kambi hizo.
M23 wadhibithi mlima Chanzu
Waasi wa M23 wamedhibithi mlima Chanzu wilayani Rutshuru ambao walikuwa wanatumia kama makao yao makuu chini ya kamanda Sultan Makenga, mwaka 2012.
Mlima wa Chanzu ulirudi mikononi mwa jeshi la DRC Novemba 5 2013 baada ya mapigano makali kwa msaada wa wanajeshi wa Malawi na Tanzania na kupelekea wapiganaji hao kukimbilia Rwanda na Uganda wakati mazungumzo kati yao na serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila yalikuwa yanafanyika.
Kundi la M23 linamshutumu rais wa DRC Felix Tshisekedi kwa kukosa kutekeleza makubaliano ya mikutano iliyofanyika Nairobi Kenya, wakati wa utawala wa Joseph Kabila.
Waasi hao walikuwa wameahidiwa msamaha kwa kufanya uasi, lakini hawana uhakika wa kupata msamaha huo kufikia sasa, kwa makosa waliofanya ya uhalifu wa vita, uhalifu dhidi ya binadamu, mauaji ya halaiki ya watu na uvunjaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
Pande zote mbili vile vile zilikubaliana kuachilia huru wafungwa, kusambaratisha kabisa kundi la waazi la M23 pamoja na kupiga marufuku uwezekano wa kundi hilo kuwa chama cha kisiasa, kurejeshwa kwa mali zilizoibwa wkaati wa vita hivyo waasi hao walipodhibithi mji wa Goma Novemba 2012.
M23 wanasema kwamba ahadi hizi hazikutimizwa na wametishia kudhibithi mji wa Goma.
Wachambuzi wanasema ni ushindani kati ya waasi
Lakini Richard Tetu, mchambuzi wa usalama eneo la maziwa makuu anasema katika mahojiano katika kipindi cha ‘kwa Undani’ cha idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika kwamba “mwanya umepatikana kwa waasi wa M23 kutekeleza mashambulizi kwa sababu sehemu hiyo inayumba kiusalama na serikali ya Congo imeshindwa kukabiliana vilivyo na kundi jingine la waasi wa Allied democratic forces ADF. Waasi hawa wamegundua kwamba jeshi la Congo halina nguvu katika sehemu hiyo na sasa ndio mda wao kusikika na kurejea mezani kushinkiza wanayotaka.”
Wataalam wa usalama wameonya kwamba mapigano ya sasa yanaweza kuyumbisha sana DRC na hata kusababisha mgogoro mkubwa wa usalama katika nchi jirani.
M23, ADF, Mai mai, dhidi ya serikali
Kurejea kwa kundi la M23 kunaripotiwa wakati serikali ya rais wa DRC Felix Tshisekedi inapambana na waasi kutoka Uganda wa Allied democratic forces ADF Kivu kaskazini.
Wachambuzi wa usalama wanasema kwamba mapigano ya M23 huenda yakavuruga mipangilio yote ya serikali kupambana na ADF.
“sasa kuna ushindani kati ya makundi ya waasi. Kila kundi linataka litambuliwe kwamba lina nguvu na ndilo linalosumbua zaidi serikali. Makundi haya yote yana lengo la kuipindua serikali ya Congo. Sasa kila kundi linataka liwe ndio limetimiza lengo hilo. Ni ushindani kati ya M23, ADF, Mai mai na mengine kuchukua madaraka.” Amasema Richard.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekuwa akitafuta ushirikiano wa serikali ya DRC, baraza la usalama la umoja wa mataifa na viongozi wengine wa maziwa makuu, kuruhusu jeshi la Uganda UPDF kuingia DRC kupambana na waasi ambao amesema unatishia usalama wa taifa la Uganda.
Kulingana na wachambuzi, Serikali ya Congo inastahili kuimarisha jeshi lake na kushirikiana na nchi jirani kukabiliana na makundi ya waasi.
Mnamo mwaka 2012, mapigano kati ya kundi la M23 na wanajeshi wa serikali ya DRC yalipelekea watu zaidi ya 100,000 kukosa makao na kusababisha mgogoro mkubwa wa hali ya kibinadamu.
Juhudi zetu za kuzungumza na waakilishi wa waasi wa M23, na viongozi wa serikali pamoja na jeshi la DRC hazikufanikiwa.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC