Vyama vya wafanyakazi vya Nigeria vinasema mgomo wa nchi nzima utaendelea jumatatu baada ya mazungumzo na serikali juu ya bei za mafuta ya petroli kushindikana.
Wawakilishi wa vyama hivyo pia walitangaza wamesitisha kitisho cha awali kusimamisha uzalishaji mafuta.
Wakati wa mazungumzo Jumamosi viongozi wa vyama vya wafanyakazi wameitaka serikali kurudisha bei za mafuta ya petroli kama ilivyokuwa kabla ya dola bilioni 8 kuondolewa katika ruzuku ya mafuta mwanzoni mwa mwezi huu. Baada ya saa kadhaa za mvutano pande hizo mbili zilimaliza mazungumzo bila makubaliano.
Raundi nyingine ya mazungumzo ilikuwa ikitazamiwa kuanza jumapili.
Kwa hivi sasa wanigeria wamekuwa wakikimbilia madukani na sokoni ili kujaza vyakula na kukuta bei zimepanda mno katika baadhi ya maeneo kufikia hadi mara tatu.