Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 16:01

Vita dhidi ya ufisadi vyapamba moto Kenya


Rais Uhuru Kenyatta akihutubia sherehe za Jamhuri Day 2016. Aliahidi kupambana na maafisa wafisadi nchini kwenye serikali yake kati ya mambo mengine.
Rais Uhuru Kenyatta akihutubia sherehe za Jamhuri Day 2016. Aliahidi kupambana na maafisa wafisadi nchini kwenye serikali yake kati ya mambo mengine.

Huku serikali ya Kenya kwa mara nyingine ikionekana kuandamwa na zimwi la ufisadi hususan kwenye taasisi ya taifa ya huduma kwa vijana, NYS, ambako takriban Shilingi bilioni tisa zimeripotiwa kufujwa, waziri wa Masuala ya umma, vijana na jinsia  Margaret Kobia Jumatatu aliwapa likizo ya lazima maafisa kadhaa wa shirika hilo.

Kati ya waliaogizwa kufanya hivyo ni wasimamizi wa idara za ununuzi na uagizaji, fedha na uhasibu. Haya yamejiri siku chache tu baada ya rais Uhuru Kenyatta kupokea barua za kujiondoa kwakKatibu mkuu wa wizara hiyo ya Vijana Lilian Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo ya NYS Richard Ndubai ili uchunguzi uendelezwe kwa njia rahisi.

Kujiondoa kwa katibu mkuu wa wizara ya vijana Lilian Mbogo Omollo na mkurugenzi mkuu wa NYS, Richard Ndubai kwa kipindi cha miezi mitatu kuruhusu Idara ya upelelezi wa jinai na tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC kukamilisha uchunguzi wake dhidi ya sakata ya NYS ambayo imeitikisa serikali ya rais Uhuru Kenyatta kwa mara nyingine kumeibua masuali mengi ya jinsi fedha za umma zimedaiwa kufujwa mara kwa mara na taasisi hii.

Na japo Bi. Omollo alieleza kuwa hicho kiwango cha fedha sicho kilichofujwa kupitia barua aliyomwandikia waziri Margaret Kobia, inadaiwa kuwa maafisa wakuu wa taasisi ya NYS walishirikiana kupora mali ya umma kwa kusaka kampuni ambazo ni bandia, kughushi stakabadhi muhimu ili kupata zabuni za mabilioni ya pesa kupitia mtandao wa kidigitali wa serikali, almaarufu IFMIS, kwa njia ambayo ni ya kilaghai.

Wiki iliyopita, Waziri wa Utumishi kwa Umma,Vijana na Jinsia Margaret Kobia, alifika mbele ya kamati ya bunge la kitaifa ya leba na kuelezea anayoyafahamu kutokana na kashfa hii na kusisitiza kuwa uchunguzi umekuwa ukiendelea na hivyo kuhitaji muda zaidi kwa uchunguzi kubaini kilichojiri.

Wakati akiwahutubia makatibu na maafisa wengine serikalini wakati wakila kiapo miezi mitatu iliyopita katika ikulu ya Nairobi,Rais Uhuru Kenyatta alikiri peupe kuwa hatomvumilia afisa yeyote anayefuja rasilimali za umma.

Maafisa zaidi ya arobaini akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi wa Umma na Vijana aliyesimamishwa kazi Lilian Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai wameagizwa leo kufika mbele ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kuelezea yale wanayoyafahamu kwenye kashfa hii ili kuvifanikisha vyombo vya usalama kubaini iwapo kulikuwapo ubadhirifu wa fedha za umma.

Awali Kamati ya bunge la Kenya kuhusu hhasibu inayoongozwa na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi imeanza kuwaagiza mashahidi na baadhi ya maafisa wa Wizara ya Vijana na taasisi ya NYS kufika mbele yake kueleza wanachokifahamu kuhusu sakata hiyo ambayo imeibua hisia chungu nzima miongoni mwa wakenya. Hapa huyu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Opiyo Wandayi.

Pia, vuguvugu la wabunge vijana katika bunge la Kenya, limewashtumu vikali maafisa ambao wametajwa kwa kufuja fedha katika wizara ya vijana.

Hii si mara ya kwanza fedha za umma zimefujwa katika taasisi ya NYS, Mwaka 2016, zaidi ya shilingi bilioni 1.8 ziliripotiwa kufujwa huku aliyekuwa waziri wa Ugatuzi wakati huo Anne Waiguru ambaye sasa ni gavana wa jimbo la Kirinyaga akilazimika kujiuzulu na wengine waliotajwa katika sakata hiyo wakiachiliwa kwa dhamana na mahakama.

Sakata ambayo ilijenga nyufa katika serikali ya rais Kenyatta huku naibu rais William Ruto wakati huo akizungumza kwa ukali.

-Imeandikwa na mwandishi wa Sauti ya Amerika, Kennedy Wandera, akiwa Nairobi.

XS
SM
MD
LG