Viongozi wa mataifa tajiri duniani na yale yanayoinukia katika kundi la G-20 wanadai kufikia makubaliano muhimu wakati wa mkutano wao wa siku mbili huko Seoul, Korea ya Kusini Rais Lee Myung-bak wa Korea ya Kusini amesema viongozi wamekubaliana na tangazo la Seoul la kuchukua hatua ya kutanzua mvutano wa sarafu.
Akitoa tangazo la mwisho wa mkutano Rais Lee alisema viongozi wamekubaliana kuacha masoko kuamua viwango vya sarafu, na wakati wanatafuta njia za kushughulikia uchumi wao ni lazima kuzingatia matatizo ya kiuchumi ya matatizo ya mataifa maskini.
Wajumbe wa G-20 hawakuweza kukubaliana juu ya masuala ya ukosefu wa uwiano wa biashara, na nakisi kubwa katika mataifa yanayoagizia kutoka nje kama Marekani, na yenye ziada katika usafirishaji nje kama vile China na Ujerumani, walipoanza mazungumzo yao.
Taarifa ilizungumzia pia haja ya kuimarisha juhudi ili kukamilisha duru ya Doha ya majadiliano ya biashra. Msemaji mmoja wa serikali ya China amesema mataifa yanayoinukia ni lazima yawe na sauti kubwa zaidi katika taasisi za fedha duniani.