Viongozi wa kisiasa wanaotoka karibu na ziwa Victoria, wameomba sheria za sasa kuhusu uvuvi na matumizi ya maji katika ziwa hilo kufutwa na badala yake sheria mpya zitungwe.
Viongozi hao wanasema sheria za sasa, haziwafaidishi watu wanaoishi karibu na ziwa na ni nchi chache zinazonufaika na rasilmali za kwenye ziwa.
Mwandishi wa VOA Kampala Kennes Bwire amesema baada ya mgogoro wa muda mrefu kuhusu uvuvi katika ziwa Victoria, viongozi wa kisiasa kutoka maeneo yaliyo karibu na ziwa hilo; Uganda na Kenya, wameanzisha mikakati ya kurekebisha sheria zinazotumika sasa kuhusu raslimali za ziwa hilo.
Katika mkutano wa pamoja mjini Sioport, kaunti ya Busia nchini Kenya, Waziri msaidizi wa jumuiya ya Afrika Mashariki wa Uganda John Maganda, amekiri kuwepo mgogoro kuhusu uvuvi na matumizi ya maji kutoka ziwa Victoria, huku wavuvi wa Kenya wakielezea kukerwa na hatua ya polisi wa Uganda kuwakamata.
“Ziwa Victoria ni mali ya jumuiya ya Afrika Mashariki. Tunapata samaki, tunalitumia kwa usafiri kutoka Jinja nchini Uganda hadi Kisumu, kenya na mpaka Mwanza, Tanzania. Hivyo tunataka wanaoutumia ziwa hilo kuwa huru,” amesema waziri Maganda
Mbunge wa Funyula nchini Kenya, Paul Otwoma anataka sheria zinazotumika kusimamia matumizi ya ziwa Victoria kuwa sawa, bila upendeleo wa nchi yeyote.
“Samaki hawajui mipaka. Samaki wanaruka tu. Wanazaliwa huku, wanaenda kule, zile sheria ambazo zimewekwa, lazima ziwe na usawa kwetu sote. Sheria za Afrika Mashariki kuhusu uvuvi zinastahili kuwa sawa kote Afrika Mashariki kuwezesha leseni moja itumike kwa wavuvi wote bila kuzingatia nchi wanayotoka. Watu wetu hawana vifaa vya kutambua mipaka iko wapi wanapovua,” amesema Otuoma.
Viongozi hao hata hivyo wanataka wavuvi kutoka nchi tatu zinazofaidika na ziwa Victoria; Uganda, Kenya na Tanzania, kuacha kuvua samaki wachanga na utumiaji kemikali katika uvuvi, wakisema hiyo ndiyo sababu kubwa polisi wengi wa Uganda wanafanya doria ziwani humo
“Polisi wanafanya doria ziwa Victoria ili kukabiliana na uhalifu na uvuvi mbaya. Tunataka wavuvi kuvua samaki waliokomaa na wala sio wachanga. Ni vyema pia kujua kiwango cha samaki wanaouzwa nje ya Afrika mashariki” ameongeza Bw. Maganda.
Matumizi ya ziwa Victoria yameshuhudia mzozo mkali kati ya nchi zinazogawana raslimali hiyo. Uganda inadai ina mgao mkubwa wa bahari hiyo kuliko Kenya, kiasi cha nchi hizo mbili kuzozana juu ya kisiwa kidogo cha Migingo.
Kwa upande wake Rais Museveni anadai maji yanayozunguka kisiwa hicho ni ya Uganda lakini kisiwa kipo Kenya.
Katika siku za karibuni wavuvi kadhaa kutoka Kenya walikamatwa na polisi wa Uganda na kuzuiliwa Uganda.
Kwa upande mwingine Misri nayo inataka maji yote yanayotoka ziwa Victoria kupitia mto Nile kuwa ni mali yake na nchi nyingine isiyatumie.
Mara nyingi, Tanzania haijihusishi katika migogoro hii ya matumizi ya ziwa Victoria licha ya kuwa na mgao mkubwa wa asilimia 37.5.