SpaceX, kampuni ya kibinafsi inayomilikiwa na mfanyabiashara bilionea, Elon Musk, ilikuwa imetoa chombo chake cha roketi, kwa mamlaka ya Marekani ya kuratibu safari na shughuli za anga za juu NASA, ili kusafiri hadi kwenye kituo cha kimataifa cha anga za juu, kikiwa kimewabeba manahodha wawili wa Marekani, ambao ni wataalam wa safari za anga za juu.
Mipango ya Uzinduzi huo ilisitishwa takriban dakika 17 kabla ya roketi hiyo kuruka kutoka kituo cha Kennedy Space Center, jimbo la Florida.
Hii ingekuwa mara ya kwanza kwa chombo kama hicho kurushwa kutoka kituo cha kurushia roketi hapa Marekani, kwa kipindi cha miaka tisa.
Maafisa wa NASA walisema Jumatano kwamba jaribio lingine la kurusha chombo hicho litafanyika siku ya Jumamosi wiki hii.
Awali, roketi nyingi ambazo zimekuwa zikienda kwenye kituo cha kimataifa cha anga za juu, zikiwa ni Pamoja na zile za Marekani, zimekuwa zikiondoka kutoka vituo vya Russia.
Rais Donald Trump alikuwa mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu wa serikali waliohudhuria uzinduzi huo ambao ulioahirishwa.