Kiongozi wa FDC, Dr Kizza Besigye amesema Ijumaa umiliki wa ardhi unaotaka kufanywa na viongozi wa serikali sio kwa ajili yamanufaa ya taifa bali ni mbinu ya viongozi hao kunyakua ardhi hiyo.
Hata hivyo alitoa mifano kadhaa ya ardhi iliyochukuliwa na serikali kwa nguvu lakini serikali hatimaye inawaachia watu binafsi kusajili ardhi hiyo.
Dkt Besigye amesema tumependekeza mambo sita katika mpango wetu tunaotaka kuutekeleza.
“Jambo la kwanza ni kukataa kabisa jaribio lolote la kufanyia marekebisho ibara ya 26 ya Katiba,” akiongeza kuwa ni lazima nchi nzima kukataa jambo hilo, na umiliki wa maeneo makubwa ya ardhi ni lazima usitishwe mara moja.
Dr Besigye amewataka wananchi waungane pamoja ili kuzuia unyakuzi holela wa ardhi.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ameripoti kuwa wizara ya ardhi kupitia gazeti la serikali imetangaza hatua ya serikali kutaka kumiliki ardhi kwa nguvu inatokana na kukwama kwa miradi ya serikali katika maeneo kadhaa nchini. Uamuzi huo umetokana na wananchi pia kukataa kuiuzia serikali ardhi zao.
Alipoulizwa na VOA kuhusu sakata hilo la ardhi, msemaji wa serikali Kanali Shabani Bantariza alikataa kuhusishwa na suala lenye utata mkubwa na hivyo kukata simu kwa haraka.
“Ili kuwawezesha wananchi kuilinda ardhi yao, hata kama wanataka kuiuza basi ni lazima wawe wanajua mambo yanayohusu bei na nyaraka,” alisema Dkt Besigye.
Alifafanua kuwa kwa sasa anayeamua bei ni afisa wa serikali na serikali ndiyo mnunuzi.
Dr Bisgye ametaka raia kutumia nguvu na mbinu zote kupinga hatua ya serikali kunyakua ardhi yao.
Amesisitiza kwamba wananchi ni lazima wawe na ufahamu wa kutosha kuhusu sheria za ardhi na haki za kuzimiliki.
Nchini Uganda unapozungumzia migogoro ya ardhi ni jambo linalofungamana na vita na mapigano.