Seneta mmoja wa Marekani ambaye kwa muda mrefu ameitaka Marekani kujihusisha barani afrika, anatetea upelekaji wanajeshi 100 wa Marekani huko Afrika ya kati kusaidia kupambana na kiongozi wa kundi la msituni.
Seneta James Inhofe kutoka jimbo la Oklahoma alisema Jumatatu kundi la Lord’s Resistance Army-LRA, na kiongozi wake Joseph Kony, kwa miaka 25 limekuwa likiwakandamiza watu nchini Uganda, Jamhuri ya Afrika ya kati, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Inhofe alimwita Kony ni mtu wa kutisha na mwenye wazimu na alionyesha picha ya wanaume vijana ambao masikio, pua, midomo na mikono ilikatwa pale walipokataa kujiunga na LRA.
Idadi kadhaa ya wanasiasa nchini Marekani na wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanamkosoa Rais Barack Obama kwa kupeleka wanajeshi Afrika ya kati.
Mgombea urais wa zamani John McCain, kiongozi wa juu wa Repuplican kwenye kamati ya seneti ya huduma za kijeshi, Jumapili alionya kuwa itakuwa hatari kujihusisha. Alisema mauaji ya Oktoba mwaka 1993 ya wanajeshi 19 wa Marekani ambao walijaribu kuisaidia serikali kuu ya Somalia kupambana na waasi.Wanajeshi kadhaa waliburuzwa katika mitaa ya mji mkuu, Mogadishu.
Lakini Inhofe anasema majeshi ya Marekani huko Afrika ya kati hayatakiwi kujihusisha katika oparesheni yeyote ya kupigana na atashauri na kuunga mkono majeshi ya eneo kufanya vyema katika mapigano.