Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:45

Marekani kuiondoa Sudan katika orodha ya wafadhili Ugaidi


Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo akiwasili Khartoum, Sudan, Aug. 25, 2020.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo akiwasili Khartoum, Sudan, Aug. 25, 2020.

Sudan imekuwa katika orodha ya Marekani ya nchi zinazofadhili ugaidi tangu miaka ya 90 na kusababisha vikwazo vya kiuchumi ambavyo vimeathiri uchumi wa nchi hiyo kwa miaka mingi hasa wakati wa utawala wa rais wa zamani Omar al-Bashir

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok amemshukuru Rais Donald Trump wa Marekani kwa hatua yake ya kutangaza kwamba yupo tayari kuiondoa Sudan katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi duniani.

Kupitia mtandao wa Twitter, Hamdok amesema kwamba hatua hiyo inakuja baada ya Sudan kukubali kulipa fidia kwa waathirika wa shambulizi la kigaidi nchini Marekani, ni nzuri sana kwa Khartoum.

Rais Trump, ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba “hatimaye haki imepatikana kwa wamarekani na ni hatua kubwa kwa Sudan”, akiongezea kwamba serikali ya mpito ya Sudan imekubali kulipa dola milioni 335 kama fidia kwa waathirika wa mashambulizi ya kigaidi na familia zao.

“Mara tu Sudan itakapotoa pesa hizo, nitaiondoa kwenye orodha ya wafadhili wa kigaidi”, ameandika Trump.

Sudan ni mojawapo ya nchi nne ambazo zimeorodheshwa na Marekani kama wafadhili wa Ugaidi.

Nchi nyingine ni Iran, Korea kaskazini na Syria.

Hatua ya kuorodheshwa kwa nchi hizo imezisababishia madhara makubwa ya kiuchumi, wawekezaji wachache wakionyesha nia ya kuwekeza katika nchi hizo.

Sudan imekuwa ikiimarisha juhudi zake za kutaka kuondolewa kwenye orodha ya Marekani kwa muda mrefu.

Iliorodheshwa baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar Al-Bashir kutangaza uhusiano na aliyekuwa kamanda wa kundi la kigaidi la Al-Qaida, Osama Bin Laden mwishoni mwa miaka ya 1990.

Nchi hiyo ambayo ina historia ya ghasia na machafuko, ilishuhudia maandamano makubwa mwaka uliopita, yaliyopelekea kuondolewa madarakani kwa Omar Al-Bashir na baadaye serikali ya mpito kuchukua hatamu za uongozi.

Utawala wa rais Donald Trump na serikali ya mpito ya Sudan, wamekuwa wakifanya mazungumzo kuhusu Sudan kuondolewa kwa orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi duniani, Marekani ikitaka fidia kwa waathiriwa hasa wa shambulizi la kigaidi la mwaka 1998 dhidi ya ofisi za balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG