Marekani inaisihi Sudan kuruhusu wachunguzi huru kuingia ndani ya jimbo lake la Kordofan kusini, baada ya Umoja wa Mataifa kuripoti shutuma za uhalifu wa vita huko.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice, alisema Jumanne hali inazidi kuwa mbaya huko Kordofan kusini, ambapo majeshi yaliyo ya uhusiano na kile kilichokuwa wakati huo Sudan kaskazini na kusini yalipambana mwezi Juni. Bibi Rice alisema Marekani inafadhaishwa sana na ripoti za mauaji yaliyokithiri, mashambulizi kwa raia, makaburi ya jumla na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu.
Rice alisema utawala wa Rais Barack Obama unaunga vyema mkono mwito wa Umoja wa Mataifa wa kufanyika uchunguzi huru huko Kordofan kusini.
Ripoti iliyotolewa na ofisi za Umoja wa Mataifa za haki za binadamu Jumatatu ilisema kuanzia Juni 7 katika mji wa Kadugli, majeshi ya kaskazini yalishambulia maeneo ya raia, waliwanyonga wakazi wanaounga mkono kusini na wizi wa ngawira na uharibifu wa nyumba za raia.
Mapigano yalifuatia Sudan kusini kujitenga kutoka kaskazini hapo Julai mosi, miaka sita baada ya vita vya muda mrefu.Serikali ya Khartoum iliagiza wapiganaji wa zamani wa kusini katika jimbo kuweka silaha chini au kuhama kwenda kusini.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inalaumu unyanyasaji zaidi katika jeshi la Kordofan kusini, polisi na wanamgambo washirika.
Rais wa Sudan Omar al-Bashir anatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC kwa mashtaka ya uhalifu wa vita na mauaji ya halaiki katika mkoa wa Darfur nchini Sudan.
Marekani inaisihi Sudan kuruhusu wachunguzi huru katika jimbo la Kordofan kusini kufuatia ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya shutuma za uhalifu wa vita katika jimbo hilo