Seneta Robert Byrd, mwakilishi wa muda mrefu kuliko wote katika bunge la Marekani, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 92.
Seneta Byrd alikuwa amelazwa hospitali tangu wiki iliyopita. Mwanzoni alidhaniwa kuwa ameathirika na joto kali lililokumba eneo la Washington DC lakini ripoti zinasema hali nyingine za kiafya zilijitokeza.
Byrd alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1952 kuingia katika Baraza la Wawakilishi na baadaye akaingia katika Baraza la Seneti mwaka 1958. Amekuwa katika afya dhaifu katika miaka ya hivi karibuni lakini aliendelea na sifa yake ya kupeleka mamillioni ya dolla katika miradi ya jimbo lake la West Virginia.
Seneta Byrd alimwunga mkono kwa nguvu Rais Barack Obama katika kampeni yake ya mwaka 2008. Alisema pia kuwa anajutia misimamo yake ya zamani katika maswala ya haki za raia, ikiwa ni pamoja na uanachama wake katika kundi la kibaguzi la KKK alipokuwa kijana.