Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 07:32

Burundi: Upinzani wamteua Agathon Rwasa kugombea urais


Agathon Rwasa ambaye aliteuliwa na upinzani nchini Burundi tarehe 16 Februari 2020 kuwania urais.
Agathon Rwasa ambaye aliteuliwa na upinzani nchini Burundi tarehe 16 Februari 2020 kuwania urais.

Wafuasi wa upinzani nchini Burundi wamefurahishwa na hatua ya chama cha National Congress for Liberty (CNL) kumteua naibu wa spika wa bunge la nchi hiyo Agathon Rwasa kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa Mei mwaka huu.

Chama hicho kilitangaza uteuzi huo Jumapili kupitia ujumbe wa Twitter.

Rwasa, mwenye umri wa miaka 56, alipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe, sawa na rais wa sasa Pierre Nkurunziza, ambaye ametangaza kustaafu na hatashiriki uchaguzi wa mwaka huu.

Rwasa na Nkurunziza wanatoka jamii ya Hutu, inayopatikana katika mkoa wa Ngozi, Kaskazini mwa Burundi.

Baada ya kuteuliwa, Rwasa, amefutilia mbali kile kinachodaiwa kuwa mipango ya chama kinachotawala kufanya udanganyifu katika hesabu ya kura.

“Wakati tunajitayarisha kwa uchaguzi mkuu, inastaajabisha kusikia kwamba kuna watu wanafikiria kufanya udanganyifu katika uchaguzi huo…. Raia wa Burundi hawatawaruhusu hilo kufanyika,” amesema Rwasa.

Mwezi Januari, chama kinachotawala cha CNDD-FDD, kilimteua Evariste Ndayishimiye kuwa mgombea wake wa urais.

Ndayishimiye, aliyekuwa generali katika jeshi la nchi hiyo, pamoja na kusimamia idara inayoshughulikia masuala ya jeshi katika ofisi ya rais, alikuwa pia waziri wa mambo ya ndani na usalama.

Juhudi zetu za kufikia maafisa wa serikali kujibu tuhuma za njama ya kufanya udanganyifu katika uchaguzi mkuu, hazikufaulu.

Je, Agathon Rwasa ni nani?

  • Alizaliwa January 10 1964 katika mkoa wa Ngozi, Burundi.

  • Ni mtoto wa 7 katika familia ya watoto 14.

  • Alisomea chuo kikuu cha Burundi.

  • Alikuwa kiongozi wa chama cha waasi cha National Liberation Forces - FNL

  • Aliongoza kundi la wapiganaji la Hutu wwakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi

  • Alisaini mkataba wa amani na serikali, Septemba 2006

  • Alichaguliwa kuwa naibu spika wa bunge la Burundi July 2015

  • Amechaguliwa kuwa mgombea wa urais wa chama cha Congress for national Liberty - CNL Februari 16 2020

Burundi ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani na mashirika ya msaada yalisitisha msaada wake mwaka 2015, baada ya kutokea machafuko kufuatia uchaguzi wa mwaka 2015.

Nchi hiyo inapitia hali mgumu kiuchumi na makovu ya vita vilivyotokea miaka iliyopita.

Tangu mwaka 2015, rais Nkurunziza alipowania mhula wa tatu madarakani, katika hatua iliyokumbwa na mzozo, mamia ya raia wa Burundi wameripotiwa kuuawa katika makabiliano na maafisa wa usalama.

Polisi, maafisa wa usalama na kundi la vijana linalojulikana kama Imbonerakure, linaloungwa mkono na chama kinachotawala, vimeshutumiwa kwa dhuluma hizo, japo serikali imekuwa ikikana madai hayo kila mara.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG