Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi limewasaidia zaidi ya wakimbizi 5,000 kurejea Jamhuri ya Afrika ya Kati kutoka Congo. Shughuli hiyo ya hiari, ambayo imekatizwa mara mbili, ilianza tena siku ya Ijumaa.
Mpango huo ulisitishwa kwa mara ya kwanza Machi 2020 wakati nchi zote mbili zilifunga mipaka yao ili kuzuia kuenea kwa COVID-19. Kukatizwa kwa pili kulitokea Desemba mwaka jana wakati ghasia zilizohusiana na uchaguzi wa rais huko Afrika ya kati zilipelekea takriban wakimbizi 92,000 kukimbilia DRC.
Msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo anasema kundi la kwanza la wakimbizi 250 waliondoka kambi ya Mole hadi mji wa Zongo kaskazini magharibi mwa DRC Ijumaa iliyopita.
Anasema kundi la pili la watu 250 waliondoka kambini Jumanne asubuhi. baadaye mchana, anasema safari ya boti ya dakika 20 itawavusha wakimbizi kuvuka Mto Ubangi hadi Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya kati.
UNHCR inatoa msaada kwa wakimbizi wanaorejea pamoja na washirika wanaofanya kazi katika miradi ya kuwajumuisha tena huko Jamhuri ya Afrika ya kati ikiwa ni pamoja na elimu na kilimo. Baadhi ya wakimbizi 206,346 wa Jamhuri ya Afrika ya kati wanaishi katika kambi na jumuiya zinazowapokea katika mikoa mitatu ya DRC. Na UNHCR na washirika wanapanga kusaidia 6,500 kati yao kurejea mwaka huu.
Tangu ghasia kati ya makundi yenye silaha kuzuka mwaka 2013, zaidi ya wakimbizi 680,000 na wanaotafuta hifadhi wamekimbilia Cameroon, DRC, Jamhuri ya Congo na Chad.
Takriban theluthi moja wanahifadhiwa nchini DRC. Watu wengine 630,000 wamekimbia makazi yao ndani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.