Kuhudhuria kwa Bi Hillary Clinton na wanadiplomasia wengine wa matafa makuu kwenye kikao maalum cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne, inasisitiza wasi wasi wa Jumuia ya Kiamtaifa kuhusiana na kulega lega kwa matayarisho ya kura ya maoni, itakayo fikisha kilele utaratibu wa amani wa Sudan, kati ya kaskazini na kusini.
Licha ya ahadi za kufanya kazi kwa nia njema zilizotolewa na serikali ya Khartoum na viongozi wa utawala wa Kusini, ugomvi ungali unaendelea juu ya kuchora mpaka, hali ya baadae ya eneo lenye utajiri wa mafuta la Abyei, ambako kura ya maoni tofauti inatarajiwa kufanyika, na kupatikana fedha za kugharimia tume ya pamoja ya uchaguzi SSRC.
Katika taarifa iliyotolewa na rais wa zamu wa Baraza la Usalama waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague, anaeleza kwamba hatua za dharura zina hitaji kuchukuliwa na pande zote mbili ili kuhakikisha kura ya maoni inafanyika kwa amani, kwa wakati ulopangwa na kwa kuaminika huko Kusini na Abyei.
“Baraza la usalama lina wasi wasi kutokana na kuendelea kucheleweshwa kutolewa fedha za kugharimia kazi za SSRC kwa ajili ya matayarisho na kuendelea mbele”. Anasema Baraza la Usalama linatoa wito kwa pande zote na mataifa yote wanachama kuheshimu matokeo ya kuaminika ya kura ya maoni itakayo fanyika kufuatana na CPA na kumulika nia ya wananchi wa Sudan ya kusini na Abyei.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban ki-Moon aliongeza sauti yake katika kueleza wasi wasi huo, akisema kwamba kura isipofanikiwa huwenda hali hiyo ikachochea upya uhasama kati ya kaskazini na kusini.
Alisema kwamba Umoja wa Mataifa una matumiani ya kuimarisha kikosi chake cha kulinda amani kwa wanajeshi elfu 10 zaidi huko Sudan, ili kuongeza usalama wakati wa kura ya maoni na baada ya kipindi hicho.
Katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Bi. Clinton alisema, mwenyekiti wa kamati ya baraza la Senet jla Marekani juu ya masuala ya kigeni, John Kerry akiwa katika ziara huko Sudan mapema mwezi huu, aliwasilisha ujumbe maalum wa rais Barack Obama unaopendekeza kwa Khartoum juu ya kuimarisha ushirikiano kati yao, pamoja na kurudisha uhusiano wa kawaida ikiwa itaamua kufuata njia ya amani.
“Ikiwa itatanzua mustakbali wa Abyei, ikiwa itaanda kura ya maoni ya Sudan ya kusini hapo Januari 9 na hapo tena kutambua matakwa ya wananchi wa Sudan kusini, basi Marekani iko tayari kuanza utaratibu wa kuiondoa Sudan kutoka orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi, utakaofuata sheria za Marekani juu ya ugaidi.”