Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 01:09

Ujumbe wa Muhoozi umeiweka Uganda katika matataizo na Sudan, DRC


Mkuu wa jeshi la Uganda Lt. Generali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa rais Yoweri Museveni. May 7, 2022.
Mkuu wa jeshi la Uganda Lt. Generali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa rais Yoweri Museveni. May 7, 2022.

Sudan inaitaka Uganda kuomba rasmi msamaha kutokana na kile imekitaja kuwa ujumbe wa kuchukiza na hatari ulioandikwa na mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba, aliyetishia kuivamia Khartoum kijeshi.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vile vile imemuita balozi wa Uganda nchini humo, kutokana na ujumbe wa Kainerugaba ambapo ametishia pia kuivamia mashariki mwa DRC.

Kainerugaba, mtoto wa rais Yoweri Museveni, aliandika ujumbe kwenye mtandao wa X Jumanne, akitishia kuivamia na kuiteka Khartoum kwa msaada wa rais mteule wa Marekani Donald Trump, atakapoingia ofisini.

Baadaye aliufuta ujumbe huo.

Sudan, kupitia taarifa ya wizara ya mambo ya nje, imesema ni lazima serikali ya Uganda iombe msamaha kutokana na ujumbe wa Muhoozi na kwamba ujumbe kama huo haustahili kutoka kwa kamanda wa jeshi.

Taarifa hiyo inataka umoja wa Afrika, na mashirika ya kikanda kulaani matamshi ya Kainerugaba, ikisema ni tishio kubwa la usalama na matuzi kwa waafrika. Sudan imeongezea kwamba matamshi hayo yamekosa busara na uajibikaji wala kutojali sheria za kimataifa, hayafuati kanuni zinazohusu ushirikiano baina ya nchi na heshima kati ya watu. Isitoshe, yanatishia vita, yanavuruga uhuru wa nchi, yanakiuka kanuni za umoja wa mataifa, umoma wa Afrika na yanastahili kuchukuliwa kwa uzito mkubwa.

DRC inataka ufafanuzi kutoka kwa balaozi wa Uganda

Muhoozi vile vile yupo katika matatizo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. DRC imemuita kaimu balozi mdogo wa Uganda nchini humo Matata Twaha Magara kutaka ufafanuzi wa maandishi ya Kainerugaba kumhusu rais Felix Tshisekedi na madai ya kuwepo mamluki mashariki mwa DRC.

Kainerugaba aliandika msururu wa ujumbe kwenye X ikiwemo onyo kwamba atawavamia mamluki walio mashariki mwa DRC kuanzia Januari tarehe 2 mwaka 2025, katika sehemu ambazo mamluki hao wanadaiwa kuwepo, ambako anadai wapo sehemu walipo wanajeshi wa Uganda UPDF, mashariki mwa DRC.

Ujumbe wake uliongezea kwamba anaapa kwa jina la mwenyezi mungu kwamba hakuna mamluki watabaki hai mashariki mwa DRC.

Je Kuna mamluki mashariki mwa DRC?

Kuna watu ambao serikali ya DRC iliwataja kama wataalam wanaotoa mafunzo ya kijeshi, kutoka kundi la Agemira, kutoka Bulgaria na kundi la RALF kutoka Romania ambao wamekuwa wakilisaidia jeshi la FARDC kupambana na waasi wa M23 tangu mwaka 2022.

DRC imekuwa ikisema kwamba watu hao sio mamluki bali wanatoa tu mafunzo kwa jeshi la FARDC.

Kainerugaba, amekuwa na hulka ya kuandika ujumbe kwenye X, wenye utata kila mara. Alipokuwa kamanda wa wanajeshi wa ardhini, alitishia kuvamia Kenya na kuteka Nairobi kijeshi hatua iliyopelekea rais Yoweri Museveni kumfuta kazi kabla ya kumteua kuwa kamanda mkuu wa jeshi la Uganda.

Forum

XS
SM
MD
LG