Leo ni siku ya uhuru nchini Uingereza. Siku hii imekuwa ya kipekee kwa sababu masharti yote ya kijamii kama vile kuvaa barakoa na kuendelea kutokaribiana kati ya mtu mmoja hadi mwingine masharti yaliyowekwa kwa ajili ya mapambano dhidi ya COVID-19 yameondolewa.
Mabadiliko ya masharti yanafanyika huku kukiwa na ongezeko katika kesi za COVID na watu kulazwa hospitali huko Uingereza kwa kiasi kikubwa kunatokana na aina mpya ya virusi vya Covid vya Delta.
Siku ya uhuru pia inatokea wakati Sajid Javid, Waziri wa afya wa Uingereza amejitenga kwa sababu alipimwa na kukutwa ana COVID. Huduma ya taifa ya afya iliwajulisha Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson, na Rishi Sunak, waziri wa fedha kwamba walikaribiana na mtu ambaye alipimwa na kugundulika ana COVID-19.
Viongozi hao wawili ambao wamejulishwa na NHS juu ya kukaribiana na mtu aliyepata maambukizi wanatarajiwa kujitenga. Hata hivyo, Johnson na Sunak walitarajiwa kushiriki katika program ambayo itawaruhusu kufanya kazi kwenye majengo ya Downing Street lakini waliamua kupinga hilo baada ya mzozo wa umma.