Ilikuwa ni ziara rasmi ya kwanza nchini Marekani kwa rais Kenyatta tangu aingie madarakani. Kenyatta na mkewe Margaret walilakiwa kwenye ikulu na Rais Trump na mkewe Melania kabla ya kikao cha wajumbe kutoka pande zote mbili ambapo masuala kadhaa yalijadiliwa, yakiwemo uwekezaji, biashara na usalama.
Trump, akizungumzia baadhi ya Nyanja za ushirikiano, alisema Marekani itashiriki katika ujenzi wa barabara kubwa nchini Kenya..
"Tunafanya mipango ya mradi mkubwa wa ujenzi wa miundo msingi. Barabara kubwa ambayo itakuwa kielelezo na mfano wa kuigwa. Tuko na wajumbe walioandamana na rais Kenyatta na tutatia saini makubaliano kadhaa ya kuzinufaisha nchi zote mbili…na ni heshima kubwa kwa rais na mkewe kuzuru ikulu," alisema rais Trump.
Kenyatta alisema kwamba ili kufanikisha azma nne kuu ambazo ameahidi kuzipa kipau mbele katika muhula wake wa pili na wa mwisho kama rais, zikiwemo afya kwa wote, makazi nafuu, lishe ya kutosha na utengenezaji wa bidhaa na vifaa, ni muhimu kwa Kenya kuwa na mazingira mema ya kuwavuta wawekezaji kutoka nchi kama Marekani.
Kenyatta alimweleza mwenzake jinsi Kenya inavyodhamini ushirikiano wake na Marekani.
"Kenya na Marekani zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na imara tangu tulipopata Uhuru. Tuko hapa kuuimarisha uhusiano huo. Na tuna ushirikiano mwema hususan katika kupambana na ugaidi na hasa kwa sababu ya ujirani wetu. Tunaendelea kupambana na al-Shabab, ambapo Marekani imekuwa mshirika mkubwa na wa karibu. Cha muhimu Zaidi ni kuimarisha ushirikiano wetu wa kibiashara ambao tayari uko imara. Tuna makampuni mengi ya Marekani nchini Kenya. Tunataka kuona jinsi ya kuimarisha ushirikiano huo kwa faida ya nchi zote mbili," alisema rais huyo.
Pembeni mwa mkutano kwenye ikulu, Serikali ya Kenya ilitia saini makubaliano ya zaidi ya shilingi bilioni 25 na makampuni mbalimbali ya Marekani, ambayo yameanzisha au yataanzisha miradi kadhaa ya uwekezaji katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Kiasi kikubwa cha uwekezaji huo kikiwa ni katika Nyanja ya umeme na kilimo.
Kenyatta amekuwa rais wa pili kutoka nchi ya bara la Afrika chini ya jangwa la Sahara kualikwa na Trump kwenye Ikulu, tangu kuiongozi huyo wa Marekani kuwa rais. Wa kwanza alikuwa Muhamadu Buhari wa Nigeria.
Rais Kenyatta aliandamana na ujumbe mkubwa wakiwemo mawaziri, maseneta, wabunge na wafanya biashara katika sekta mbalimbali.