Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 06:06

Uhuru Kenyatta asifu utendakazi wa serikali yake wakati wa sherehe za Madaraka


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. PICHA: AFP
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. PICHA: AFP

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Jumatano ameliongoza taifa kuadhimisha miaka 59 ya nchi hiyo kupata uhuru wa kujitawala, maarufu kama Madaraka Day.

Haya yakiwa ni maadhimisho ya mwisho ya kitaifa katika utawala wake, Kenyatta kando na kutumia muda mwingi katika hotuba yake kuelezea mafanikio mengi ya serikali yake, amependekeza kuwa serikali ijayo ni sharti ipambane na ufisadi ndani na nje ya serikali kuipatia Kenya mafanikio makubwa.

Baada ya kutwaa madaraka Aprili 9, 2013 kuwa rais wa Kenya, wa awamu ya nne ya Jamhuri, rais Kenyatta, miaka tisa na miezi miwili baadaye, ametumia maadhimisho haya katika bustani ya kihistoria ya Uhuru jijini Nairobi paliposhushwa bendera ya mkoloni Mwingereza na kupeperushwa bendera ya Jamhuri ya Kenya usiku wa manane wa Desemba 12, 1963 na kuchezwa wimbo wa taifa kwa mara ya kwanza, kuelezea mafanikio yaliopatikana na utawala wake.

Kenyatta asifu utawala wake

Mwanzo, Kenyatta ameeleza kuridhishwa na jinsi serikali yake ilivyokuza uongozi wa wanawake katika matawi ya serikali kudumisha usawa na ushirikishwaji wao katika maamuzi muhimu ya nchi.

Kutoka kwa jaji mkuu Martha Karambu Koome—Mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, Kenyatta amewateua mawaziri wanawake kumi na mmoja katika baraza lake la mawaziri katika nyakati na nyadhifa tofauti, na kwamba sasa Kenya ina chaguo la kumpata naibu rais wa kwanza mwanamke katika uchaguzi ujao.

Akiashiria Martha Karua ambaye ni mgombeamwenza wa Raila Odinga.

“Mnamo Agosti mwaka huu, ikiwa ni matakwa ya wapiga kura, tuna nafasi ya mwanamke kuvunja kizuizi kwa kushika wadhifa wa pili wa juu katika Jamhuri yetu, Ofisi ya Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya”

Ujenzi wa taifa

Kenyatta, anasema kuwa serikali yake imejikita sana katika kufaulisha vigezo vinne vya maendeleo makubwa ya nchi ikiwa ni Kuongeza Kasi ya maendeleo ya Kiuchumi, Urejesho wa Utu, na Uimarishaji wa Kisiasa na katika misingi hiyo, utawala wake umejenga barabara za lami zenye zaidi ya urefu wa kilomita 11,000, ambayo ni karibu mara sita ya zile serikali zilizopita pamoja, ikiwa ni pamoja na wakoloni, zilizojenga katika miaka 123.

Kenyatta, aidha anaeleza kuwa kupitia upanuzi na ukuaji wa mitandao ya kidijitali, serikali yake imewawezesha wakenya, wafanyabiashara wadogo na wa kati; kufikia masoko kwa haraka.

Aidha, anakariri kuwa mapato ya taifa ya kahawa yameongezeka maradufu na wakulima sasa wananunua kilo moja kati ya shilingi 110-125 tofauti na ilivyokuwa shilingi 60 kwa kilo mwaka 2013.

Ukuaji wa uchumi

Kenyatta anaeleza kuwa mapato ya chai kutokana na mauzo ya nje yaliongezeka kwa 20% kutoka shilingi bilioni 114 mwaka wa 2013 hadi shilingi bilioni 136 Bilioni mwaka wa 2021. Huku zaidi ya shilingi bilioni 450 zikilipwa kwa wakulima wadogo wa chai.

Rais Kenyatta, anaeleza kuwa ameiwezesha Kenya kuhama kutoka uchumi wa 12 kwa ukubwa barani Afrika, hadi kuwa wa 6 kwa uchumi mkubwa na unaokua huku pato la taifa likifikia shilingi trilioni 13 kutoka trilioni 4.5 alipotwaa madaraka. Mapato ya taifa ya ushuru yameongezeka maradufu kutoka shilingi bilioni 800 mwaka 2013 hadi shilingi trilioni 1.662 kufikia Aprili 2022 na serikali yake inakadiria kuvunja rekodi ya makusanyo ya shilingi trilioni 2 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa kifedha.

Kuhusisha jeshi katika kazi za raia

Vile vile, ametetea ushirikishwaji wa jeshi la Kenya kusimamia na kutekeleza miradi ya serikali. Akijitetea kuwa hakuwa na nia nyingine, jukumu lake lilikuwa ni kutoa maendeleo ya nchi mikononi mwa waporaji.

Miezi miwili kabla kuondoka afisini, Kenyatta, anaitaka serikali ya awamu ya tano, kuyapa kipaumbele mapambano dhidi ya ufisadi, kusuluhisha migogoro ya kisiasa na unafiki ulio ndani ya viongozi wa kisiassa wanaoshikilia nyadhifa za serikali, kuendeleza uwekezaji utakaoleta maendeleo kwa taifa.

Katika kile kilichoonekana kuwa ni kuvunja itifaki ya serikali, Kenyatta amempuuza naibu wake William Ruto ambaye angehutubia kisha kumualika na badala yake kumualika rais wa Sierra Leone Maada Bio anayezuru Kenya kwa ziara ya kiserikali.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG