Polisi wa Uganda wamefyatua gesi ya kutoa machozi kutawanya mkutano wa hadhara wa upinzani ulioitishwa kuwakumbuka watu waliouawa katika maandamano mapema mwaka huu.
Walisohuhudia wanasema watu mia kadha walikusanyika katika kitongoji kimoja cha Kampala lakini polisi wakavamia uwanja huo kabla mkutano kuanza na kutawanya umati wa watu.
Wafuasi wa upinzani wanasema polisi walitoa kibali cha kufanyika kwa mkutano huo lakini baadaye wakasema waandamanaji hawakukusanyika katika eneo lililoidhinishwa kufanyika mkutano huo.
Kiongozi wa upinzani Kizza Besigye aliyeandaa maandamano ya “Kutembea kwenda kazini’ kupinga nyongeza ya bei ya chakula na mafuta mwezi Aprili na Mei, hakuhudhuria mkutano wa leo..
Wiki iliyopita mahakama ilifutilia mbali kesi dhidi ya Besigye kwa misingi ya kutokuwepo na ushahidi wa kutosha.
Makundi ya upinzani yanalaumu sera za rais Museveni kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, lakini rais huyo anasema yote hayo yametokana na kudorora kwa uchumi duniani na kwamba kamwe hatavumilia maandamano.