Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 16:13

Uganda na WHO kujaribu chanjo mbili za virusi vya Ebola ya Sudan


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Uganda Diana Atwine, katikati, akithibitisha kisa cha Ebola nchini humo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kampala, Uganda Jumanne, Septemba 20, 2022. (AP).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Uganda Diana Atwine, katikati, akithibitisha kisa cha Ebola nchini humo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kampala, Uganda Jumanne, Septemba 20, 2022. (AP).

Uganda na Shirika la Afya Duniani-WHO wanapanga kujaribu chanjo mbili za virusi vya Ebola ya Sudan ili kujaribu kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nadra.

Virusi hivyo hadi sasa vimewauwa watu 19 na kuwaambukiza takriban watu 54 katika wilaya tano nchini Uganda. Baada ya mikutano mjini Kampala, mkurugenzi mkuu wa WHO alielezea mlipuko huo mpya kama unaotisha.

Uganda iliwakaribisha mawaziri kutoka nchi 11 katika mkutano wa dharura wa siku moja Jumatano ili kujiweka sawa katika maandalizi yao na kukabiliana na milipuko ya Ebola na kukubaliana kuhusu mkakati wa ushirikiano.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Dk. Jane Ruth Aceng, waziri wa afya wa Uganda, alisema idara hiyo inatarajia aina mbili tofauti za chanjo ya virusi vya Ebola vya Sudan vinavyosambaa kwa sasa nchini Uganda.

Chanjo zote mbili, kulingana na WHO, zinasubiri idhini ya udhibiti na maadili kutoka serikali ya Uganda. Aceng anasema chanjo hizo zinazotarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo ziko katika majaribio ya kimatibabu.

Uganda iliripoti mlipuko wa Ebola Septemba 20. Kitovu chake ni wilaya ya Mubende, magharibi mwa Kampala, huku kifo kimoja kikiripotiwa Kampala kwenyewe.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema ingawa mlipuko huo unatisha sio jambo ambalo halikutarajiwa. Tedros anasema lengo la msingi sasa ni kudhibiti mlipuko huo ili kulinda wilaya jirani, na pia nchi jirani.

WHO iliwataka majirani wa Uganda kuongeza utayari wao wa kujibu haraka na kwa ufanisi, ikiwa itahitajika.

Dk. Ahmed Ogwell Ouma, kaimu mkuŕugenzi mkuu wa Vituo vya Afŕika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, anasema nchi za Afŕika zinahitaji kubadili jinsi zinavyofanya mambo wakati wa milipuko.

Alisema hii ni pamoja na kuimarisha taasisi zinazohusika na dharura za afya, kuimarisha nguvu kazi ya afya, viwanda vya ndani na kuwa na ushirikiano wenye mwelekeo na heshima.

WHO imetoa dola milioni 2 kutoka kwenye hazina yake ya dharura ili kusaidia Wizara ya Afya ya Uganda na dola milioni 3 za ziada kusaidia utayari katika nchi jirani.

Ogwell anasema fedha hizo zinahitaji kupewa kipaumbele.

"Si weli kwamba hatuna pesa. Na si kweli kwamba nchi za Kiafrika hazina fedha. Ni suala la kuweka kipaumbele kwa rasilimali ulizo nazo. Na kisha, washirika wanapoleta msaada wao, inasaidia nini? Je, ni kusaidia vipaumbele vyetu au ni kusaidia kipaumbele cha mshirika? Kisha, urekebishaji wa bajeti zetu katika ngazi ya kitaifa utaleta hali ambapo fedha za sekta ya umma zinaingia katika vipaumbele vyetu" aliongeza Ogwell.

Virusi vya Ebola vya Sudan viliripotiwa kwa mara ya kwanza kusini mwa Sudan mwaka 1976. Milipuko kadhaa imeripotiwa tangu wakati huo nchini Uganda na Sudan. Mlipuko mbaya zaidi nchini Uganda ulikuwa mwaka wa 2000 na kuua zaidi ya watu 200.

XS
SM
MD
LG