Serikali ya Uganda imekataa kufanya mazungumzo na vyama vya upinzani ili kumaliza sintofahamu ya kisiasa iliyolikumba taifa hilo.
Serikali badala yake inasema upinzani usubiri uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2021 huku upinzani ukitishia kuuangusha utawala wake rais Yoweri Museveni.
Mwandishi wetu wa Kamapala, Kennes Bwire anaripoti kuwa Dkt. Kiiza Besigye na chama chake cha FDC, wanashikilia kuwa mazungumzo kati ya wanasiasa wa upinzani na utawala wake rais Museveni, ndiyo hatua ya mwisho ya kile alichokiita kuikomboa Uganda.
Besigye anafafanua kwamba hali ya kisiasa nchini Uganda siyo swala la uadui kati yake na rais Museveni, bali ni kwa manufaa ya Uganda, akisema nchi imepoteza mwelekeo, na raia wake wamegawanyika, huku utawala ukitumia risasi kuwanyamazisha.
“Tunapozungumza kuhusu mazungumzo ya kisiasa, tunawashauri tu. Ni kwa manufaa yao. Yanayofanyika nchini kama mauaji ya Kasese ni ishara kwamba tunaelekea katika matatizo makubwa. Nina imani kwamba walio madarakani wataangushwa,” alisema Dkt Besigye.
Lakini katibu mkuu wa chama tawala cha NRM, Kasule Lumumba, anasema mazungumzo anayotaka Besigye na chama chake hayatafanyika. Badala yake anataka wafuate sheria.
Msimamo wa chama tawala cha NRM ni sawa na ule wa msemaji wa serikali Ofwono Opondo, ambaye naye anasema kwamba iwapo Besigye na chama chake cha FDC wanataka kuitawala Uganda, waimarishe chama chao wakisubiri uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.
“Jiandae kwa uchaguzi mkuu wa 2021 ili wakati huo utakapofika wengi wa wapiga kura wataamua iwapo ni nyinyi mnsatahili kuwaongoza.
Alisema ni vyema wasitumie udhaifu wao wa kushindwa kujiimarisha kisiasa kama ngao ya kuiita serikali hii ni haramu na inaongozwa na dikteta,” amesema msemaji wa serikali Ofwono Opondo
Kwa upande wao kanisa linakubaliana naye Dkt Besigye kwamba mazungumzo yanahitajika kusahihisha mambo kadhaa yanayosemekana kwenda mrama.
Askofu Zark Niringiye, anawarai viongozi wa kisiasa kukubali kwamba Uganda inauguza vidonda sugu vya ukatili wa kibinadamu, unyakuzi wa ardhi, dhuluma katika jamii, malumbano, kutoaminiana, na mengine mengi.
Askofu Ningiriye, ana mtazamo kwamba hata viongozi wa dini wamekosa kuwajibika katika maswala yanayoikumba Uganda na badala yake wamekaa kimya huku wakijua vyema kwamba kuna matatizo mengi yanayohitaji kurekebishwa kwa haraka.
“Tuna makaburi ya pamoja kila mahali. Watu wameuawa na kuzikwa kwa siri. Tumelazimisha watu kuwa wajane na yatima humu nchini. Tunahitaji ukweli na maradhiano. Tuna vidonda sugu vingi. Nchi imevunjika,” alisema askofu Zark Niringiye.
Mwanzoni mwa wiki hii, Besigye alihutubia waandishi wa habari na kufichua kwamba ameunda serikali aliyoita ya watu, na kwamba ana wafuasi wake wengi katika kila kijiji kote Uganda, wanaosubiri amri kutoka uongozi wa chama cha Forum for democratic change (FDC), kuchukua hatua za kuitawala Uganda.
Besigye anashikilia kwamba alishinda uchaguzi mkuu wa mwaka jana kwa asilimia 52 lakini Yoweri Museveni akampokonya ushindi wake.