Baryomunsi ameambia waandishi wa habari kwamba Museveni “atasaini mswada huo” na kuonya jumuiya ya kimataifa dhidi ya kile ametaja kama kuwatisha viongozi wa Uganda kwamba watawekewa vikwazo.
“Tunatunga sheria kwa ajili ya raia wa Uganda na wala sio wzungu. Kama wanataka, basi watuwekee vikwazo,” amesema Baryomunsi.
Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yamekashifu hatua ya bunge la Uganda kupitisha mswada unaoharamisha ushoga nchini humo, yakisema ni ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
Muswada uliopitishwa na bunge una hukumu ya hadi kifo kwa wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na kuambukiza wengine virusi vya ukimwi.
Watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja waatahukumiwa mika 20 gerezani, huku wale watakaopatikana wakijaribu kufanya mapenzi ya jinsia moja wakihukumiwa miaka 10 gerezani.
Waziri wa sheria na maswala ya katiba wa Uganda Nobert Mao ametaka raia wa Uganda kukataa kile ametaja kama jaribio la kuharibu mila tabia zao.
“Wakati mwingine, hawa watu wanaoitwa wafadhili, jumuiya ya kimataifa na wanaotutishia, hawatutakii mema,” amesema Mao.
Mao amesema kwamba itakuwa vigumu kwa mataifa ya magharibi kukubali mataifa ya Afrika kupeleka utamaduni wao katika mataifa hayo na kuhoji kinachopelekea kulazimisha ushoga kwa mataifa mengine.