Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 21:41

Uganda kukarabati reli ya kitambo, hakuna taarifa kuhusu SGR


Baraza la mawaziri nchini Uganda limeidhinisha mpango wa serikali wa kukarabati reli ya kitambo kutoka Malaba, mpaka wa Kenya na Uganda, hadi Kampala.

Mpango huo unazima mpango wa awali wa ujenzi wa reli ya mwendo wa wastani -SGR, na hakuna ripoti yoyote kuhusu ujenzi wake.

Taarifa iliyotolewa jumanne na kituo cha habari cha serikali, inasema kwamba ukarabati wa reli hiyo “itakuwa hatua muhimu sana katika kuimarisha shughuli ya kubeba mizigo na abiria nchini Uganda.”

Taarifa hiyo inaendelea kusema kwamba “reli hiyo itapunguza gharama ya kufanya biashara, kuimarisha mapato ya nchi, na kuboresha maisha ya raia wa Uganda.”

Ukarabati wa reli hiyo utagharimu shilingi trilioni 1.4 za Uganda na unakuja wakati Uganda inakabiliwa na gharama ghali ya kusafirisha mizigo kwa kutumia barabara.

Kwa sasa, inagharimu dola 3600 kusafirisha kasha la futi 40 kutoka bandari ya Mombasa Kenya hadi Kampala kwa kutumia barabara. Mzigo kama huo unagharimu dola 1,800.

Kulingana na muungano wa wafanyabiashara jijini Kampala – KACITA, asilimia 50 ya bei ya mizigo inayosafirishwa kutoka Mombasa hadi Kampala, ndio gharama inayotumika kwa usafiri.

Hivi karibuni, rais Yoweri Museveni alizindua ujenzi wa reli kutoka mji wa Tororo, mpakani mwa Kenya na Uganda hadi Gulu, kaskazini mwa Uganda.

Museveni alisema kwamba usafiri wa reli ambao mara ya mwisho kufika Gulu ilikuwa ni mwaka 186, utaanza tena kwa sababu Serikali yake inatambua kwamba usafiri kwa gharama nafuu ni muhimu kwa ukuaji wa biashara.

Reli kutoka Malaba hadi Kampala, yenye urefu wa kilomita 273 ni muhimu pia kwa bidhaa za Uganda zinazouzwa nje ya nchi kupitia bandari ya Mombasa.

Reli hiyo inapita katika wilaya 9 za Tororo, Butaleja, Iganda, Mayuge, Jinja, Buikwe, Mukono, Wakiso na Kampala.

Serikali imesema kwamba baada ya ukarabati wake, mizigo yote kutoka bandari ya Mombasa, ambayo imekuwa ikisafirishwa kwa kutumia barabara, itasafirishwa kwa reli ili kupunguza gharama ya usafiri na ukarabati wa barabara kila mara.

Umoja wa ulaya utasaidia serikali ya Uganda katika kufadhili ujenzi wa reli kutoka Tororo hadi Gulu, yenye urefu kwa kilomita 375.

Serikali ya Uganda pia imeanza mipango ya kufufua usafiri wa meli kutoka Kisumu Kenya hadi bandari za Kasensero na Bukakata.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG