Taarifa zinasema kwamba mji wa Shanghai pamoja na miji mingine ilifungwa kufuatia mlipuko mpya wa virusi vya corona, ikiongeza kusema kwamba kuna matumaini ya kujikwamua sasa kwa kuwa hali ya kawaida imerejea.
Hatua za kuzuia maambukizi zilipelekea kufungwa kwa Shanghai ambapo kuna bandari yenye shughuli nyingi zaidi kwenye taifa hilo la pili kwa uchumi duniani, na kuzua wasi wasi wa kuathirika kwa biashara za kimataifa pamoja na viwanda.
Mamilioni ya familia pia zililazimika kubaki nyumbani na kwa hivyo kuathiri soko la bidhaa nchini humo. Chama tawala cha kikomunisti kimeahidi misamaha ya kodi, kutolipa kodi za nyumba kwa muda, pamoja na misaada mingine ya kifedha ili kusaidia biashara kurudi kwenye hali ya kawaida.
Baadhi ya wafanyabashara wadogo kama wa migahawa na maduka wamefunga biashara zao, huku waliobaki wakilalamikia hali ngumu ya kiuchumi kutokana na janga hilo.