Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 10:13

Uchaguzi wa Mali watiliwa mashaka na ECOWAS


Wanajeshi wa Mali wakishika doria kwenye mji mkuu wa Bamako
Wanajeshi wa Mali wakishika doria kwenye mji mkuu wa Bamako

Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya afrika magharibi ECOWAS, Jumanne imesema kwamba ina wasiwasi kwamba serikali ya mpito ya Mali haija piga hatua za kutosha kuelekea uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari mwakani kama ilivyokubaliwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, ECOWAS imesema kwamba hali ya kurejea kwenye demokrasia nchini humo inafuatiliwa kwa karibu baada ya kupinduliwa kwa rais Ibrahim Boubacar Keita na hasa ikizingatiwa kwamba eneo la Afrika magharibi limeshuhudia mapinduzi mara nne, la karibuni lilifanyika Jumapili nchini Guinea.

Baada ya mapinduzi ya Mali, viongozi wa kijeshi wanaoshikilia madaraka walikuwa wakipata shinikizo kutoka kwa mataifa wanachama wa ECOWAS na hivyo kukubali kuitisha uchaguzi wa rais na bunge baada ya miezi 18. Hata hivyo kuahirishwa mara kwa mara kwa tarehe ya uchaguzi, kuchelewesha kwa uandikishaji wa wapiga kura pamoja na pendekezo la katiba mpya ni masuala yanayotia wasiwasi.

Kipindi cha mpito nchini humo kilikumbwa na tatizo jingine mwezi Mei baada ya kanali aliyeongoza mapinduzi ya kwanza Assimi Goita kuamuru kukamatwa kwa rais wa mpito, wakati yeye mwenyewe akishikilia wadhifa huo. ECOWAS imeelezea wasiwasi wake kupitia taarifa wakati wa kumalizika kwa ziara ya wajumbe wake nchini humo wakiongozwa na aliyekuwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan.

Serikali ya mpito hata hivyo imeahidi kuheshimu ahadi ya kuitisha uchaguzi, ingawa baadhi ya maafisa wanasema kwamba huenda isiheshimiwe. Mchambuzi wa masuala ya siasa Bassirou Ben Doumbia amesema kwamba muda uliopo hautoshi kuitisha uchaguzi wenye hadhi. Anasema kuwa iwapo mambo yataharakishwa, basi yatapelekea mizozo ya kawaida ambayo inajitokeza baada ya kila uchaguzi.

XS
SM
MD
LG