Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 03, 2025 Local time: 05:28

Uchaguzi wa urais Kenya kurudiwa, mahakama ya juu yaamuru


Maafisa wa IEBC
Maafisa wa IEBC

Mahakama ya juu nchini Kenya, siku ya Ijimaa ilitoa uamuzi uliokuwa umesubiriwa na Wakenya wengi na kusema kuwa ni sharti uchaguzi wa rais urudiwe katika kipindi cha siku sitini.

Wakiongozwa na jaji mkuu David Maraga, majaji hao walikuwa wakisikiliza kesi iliyowasilishwa mahakamani na aliyekuwa mgombea wa muungano wa upinzani wa NASA, Raila Odinga

Ijumaa, majaji wanne walikubaliana kwamba uchaguzi huo ulikuwa na dosari. Hata hivyo, majaji Njoki Ndung'u na Jackton Ojwang hawakukubaliana na wenzao. Jaji Mmoja Mohammed Ibrahim, hakushiriki kwenye uamuzi huo kwani alikuwa mgonjwa.

Akizungumza nje ya mahakama kuu mjini Nairobi muda mfupi baada ya uamuzi huo, aliyekuwa mgombea urais wa upinzani Raila Odinga alisema kuwa Ijumaa ilikuwa ni siku ya kihistoria kwa Kenya na kwa Afrika.

"Kwa mara ya kwanza, Mahakama imefutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais naiImetoa mfano mwema," alisema Odinga.

"Tulisema tangu awali kwamba safari yetu ya Canaan haiwezi kuzuiwa. Siku ya tarehe 8 Agosti tulivuka mto Jordan," aliongeza.

Aidha, mwanasiasa huyo alisema upinzani hauna imani kwamba tume ya sasa ilivyo inaweza kuandaa uchaguzi huru na wa haki.

"Maafisa wengine wa tume hiyo wanatakiwa kuwa jela,' alsema Odinga.

Kwa mujibu wa sheria za Kenya, sasa wagombea wote wanane walioshiriki kwenye uchaguzi wa kwanza, watashiriki katika raundi ya pili ya uchaguzi.

Punde tu baada ya uamuzi kusomwa, Wakenya katika baadhi ya maeneo waliandamana barabarani kusherehekea.

Habari zaidi zitafuata hivi punde....

XS
SM
MD
LG