Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:12

Tutawawezesha Watanzania walio nje kushiriki uchaguzi - Balozi Mulamula


Waziri wa Mambio ya nje wa Tanzania Liberata Mulamula
Waziri wa Mambio ya nje wa Tanzania Liberata Mulamula

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Balozi Liberata Mulamula amesema kwamba wizara yake iko tayari kuwawezesha Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kupiga kura endapo watapata ridhaa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, akiongeza kuwa ni rahisi kufanya hivyo kwa kutumia teknolojia.

Akizungumza na wahariri wa gazeti la Mwananch jijini Dar es Salaam, waziri huyo alisema Ijumaa kwamba serikali inalishughulikia kwa makini suala la uraia pacha na kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha, litakuwa limepatiwa ufumbuzi.

Mulamula alisema kuwa serikali ya Awamu ya Sita "imetambua suala la uraia pacha linakwenda sambamba na ushiriki wa diaspora; na watu wengi, wakiwamo wabunge, wamekuwa wakionyesha utayari wao."

Alisema haamini kwamb mtu anaweza kuondolewa haki ya kuzaliwa katika nchi aliyozaliwa, na kuongeza kuwa Watanzania wengi walio nje ya nchi wamekwenda kutafuta maisha na wako kwenye fani tofauti, ukiwamo udaktari na biashara, hivyo, wana mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.

“Tukiwa bungeni kuna mbunge mmoja aliondoa shilingi mpaka tumpe majibu, wakati ule zamani tukienda bungeni walikuwa wanasema ‘bwana wee usituambie habari za diaspora, wanakula kuku kwa mrija, wachague wanataka wapi, huwezi kupata huku ukapata kule’. Sasa mtazamo umebadilika, wao ndio wanaotaka,” alinukuliwa na gazeti la Mwannchi akisema.

“Wabunge wengi wametoka diaspora, nikawaambia kama mnalitaka hili basi, na ninyi ni watunga sheria, sisi tunalifanyia mkakati wa kisera, lakini likija kwenye sheria ninyi wabunge ndiyo mtusaidie tuipitishe,” aliongeza

“Ningekuwa na uwezo ningelimaliza hata jana, ingekuwa imenipa amani sana, hasa kukuza ushiriki wa diaspora. Mtazamo umebadilika, si kama huko nyuma, kwa hiyo mimi naamini kabla ya mwisho wa mwaka huu, tutakuwa tumelipatia suluhu hili la uraia pacha,” alisema.

Alisema suala la uraia pacha lilitakiwa lipite katika mchakato wa mabadiliko ya katiba, lakini ilionekana si suala la kuingia kwenye katiba, bali kuliwekea sheria maalumu kama zilivyofanya Ethiopia na India.

“Kubadilisha Katiba ni mchakato mrefu, lakini ikishaingia kwenye katiba halafu ukaja utawala mwingine hauitaki, unaitoaje? Kwa hiyo kukiwa na sheria inawalinda zaidi.

“Sasa tumesema tunavyoainisha hii sera yetu ya mambo ya nje, tuko kwenye mkakati wa kuweza kuja na programu maalumu wanayoita hati maalumu zinazowatambulisha Watanzania walioko nje,” alisema.

Suala la uraia pacha ni kati mwa mambo yaliyoibuka na kujadiliwa kwa upana wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) ikikusanya maoni ambayo yaliwekwa kwenye rasimu ya pili ya Katiba kisha kupitishwa kwenye Katiba inayopendekezwa.

Sehemu moja ya rasimu ya pili ya katiba inaeleza: “Bila kuathiri masharti yaliyomo kwenye sura hii, mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano kwa kupata uraia wa nchi nyingine, atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano, atakuwa na hadhi maalumu kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.”

XS
SM
MD
LG