Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu nchini Tanzania Jumatano imefuta kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, Tundu Lissu na wenzake watatu.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi hatua hiyo imekuja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Lissu na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002 ya Tanzania.
Wengine waliokuwamo katika kesi hiyo walikuwa ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.
Akizungumza na VOA Mchambuzi Sammy Ruhuza anasema DPP ana uwezo wa kuamua kuendelea na kesi hiyo au la wakati wowote kulingana na katiba ya Tanzania lakini kufutwa kwa kesi hiyo pamoja na kesi nyingine kadhaa siku za nyuma kipindi cha awamu ya 5 kunaonyesha kuwa Jamhuri hawakuwa na kesi yoyote, ilikuwa ni kesi za kubambika na huo ni unyanyasaji na kurudisha nyuma uhuru wa kujieleza nchini Tanzania.
Akipendekeza kuwa kesi nyingi zilizopo mahakamani ni za aina hiyo na zifutwe zote akiasa serikali nchini humo kuwa makini.