Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Februari 24, 2025 Local time: 01:24

Tshisekedi: Sina shaka yoyote kwamba Rwanda inawasaidia waasi wa M23


Jeshi la DRC likipiga doria katika vita dhidi ya waasi wa M23. PICHA: AFP
Jeshi la DRC likipiga doria katika vita dhidi ya waasi wa M23. PICHA: AFP

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amesema kwamba hana shaka kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana vita na wanajeshi wa DRC mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza akiwa Congo Brazzaville, Tshisekedi amesema kwamba ni “muhimu nchi kujenga uhusiano mwema na wala sio ukuta”, akiongezea kwamba “kwa bahati mbaya, tupo mahali tulipo.”

Hii ni mara ya kwanza Tshisekedi amezungumzia wazi wazi kuhusu uhusiano unaoendelea kuharibika kati ya DRC na Rwanda, baada ya waasi wa M23 kuongeza mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa serikali katika sehemu za jimbo la Kivu Kaskazini.

Tshisekedi afanya mazungumzo na Sassou Nguesso

Tshisekedi, ambaye alinusurika mapinduzi hivi karibuni, wakati alipokuwa katika ziara ya kikazi nchini Ethiopia, amesisitiza kwamba “Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 kuishambulia nchi yake.”

Kulingana na shirika la habari la AFP, Tshisekedi amesisitiza kwamba. “Hana shaka yoyote kuhusu hilo.”

Vyombo vya habari vya Uganda vinaripoti kwamba wanajeshi 17 wa DRC wameuawa kufikia sasa, katika mapigano makali kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa serikali.

Tshisekedi amesema kwamba “hatua za kuimarisha uhusiano mwema na jirani yake Rwanda, siyo fursa kwa majirani kuja kutuchokoza.”

Rwanda imekana mara kadhaa, shutuma za kuwaunga mkono waasi wa M23, lakini jeshi la DRC limesema kwamba limekamata silaha na sare za kijeshi za Rwanda.

Wanajeshi wawili wa Rwanda walikamatwa na jeshi la DRC wakiwa ndani ya DRC, lakini Kigali imesisitiza kwamba wanajeshi hao walitekwa nyara mpakani wakiwa wanapiga doria.

Kigali vile vile imeishutumu DRC kwa kuunga mkono waasi wa FDLR, wanaoshutumiwa kwa mauaji ya kimbari yam waka 1994, nchini Rwanda.

Mahojiano na msemaji wa waasi wa M23 Mj. Willy Ngoma
please wait

No media source currently available

0:00 0:12:21 0:00

Mapigano yaongezeka

Jeshi la DRC limeendelea kuwashambulia waasi wa M23. Kamanda wa waasi hao Brig Sultan Makenga, anaripotiwa kujificha Rugarama, kilomita 17 kutoka mpaka wa DRC na Uganda.

Rais wa DRC Tshisekedi amenukuliwa akisema kwamba “anadhani kwamba Rwanda imepata funzo,” baada ya jeshi la DRC kuwafurusha waasi wa M23 kutoka sehemu kadhaa walizokuwa wamezidhibithi.

Mashirika ya kutetea haki za kiraia yamefurahishwa na mashambulizi yanayotekelezwa na jeshi la DRC dhidi ya waasi wa M23.

Maelfu ya raia wa DRC waliandamana katika miji ya Kinshasa, Goma na Lubumbashi, wakidai kwamba Rwanda ilikuwa inawaunga mkono waasi wa M23.

Balozi wa Rwanda nchini DRC Vincent Karega, ambaye alikuwa ameitwa na serikali ya DRC kuhojiwa kuhusu kundi la waasi la M23, aliondolewa ofisini mwake na polisi wa DRC wakati wa maandamano hayo mjini Kinshasa.

Mpaka wa DRC na Rwanda kufungwa?

Kuna ripoti kwamba rais wa DRC Tshisekedi alikuwa ameshauriwa na maafisa wake kufunga Mipaka yote ya DRC na Rwanda, lakini viongozi wa kanda wakamshauri kutofanya hivyo.

Wiki iliyopita, Tshisekedi aliwafuta kazi maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi, wanaoshukiwa kushirikiana na Rwanda.

Viongozi wa M23 Wazungumza

Kiongozi wa kisiasa wa M23 Betranda Bisimwa, amesema kwamba jeshi la DRC, FARDC, na washirika wake wameanzisha mashambulizi makali dhidi ya M23 katika sehemu ya Jomba jumatatu asubuhi.

Jomba ni sehemu iliyo karibu na mpaka wa Uganda.

Msemaji wa M23 Maj Willy Ngoma amesema kwamba jeshi la DRC limeongeza idadi ya wanajeshi wake na silaha katika sehemu kadhaa mashariki mwa DRC tayari kushambulia ngome za M23.

Kundi la M23 linadai kwamba jeshi la DRC linasaidiwa na waasi wa FDLR.

Willy Ngoma anataka serikali ya DRC kufanya mazungumzo na kundi hilo la waasi.

“Hakuna jawabu la kijeshi kwa matakwa ya M23. Ni mazungumzo tu ndio yatamaliza vita hivi.” Amesema Ngoma.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG