Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 22:02

Tshisekedi: Raia wa Rwanda ni ndugu zetu, wanahitaji msaada kuwa huru


Rais wa DRC Felix Tshisekedi (kushoto) na wa Rwanda Paul Kagame.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi (kushoto) na wa Rwanda Paul Kagame.

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi ameonekana kumjibu mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, kutokana na matamshi kwamba kiongozi huyo wa Congo huenda anasababisha mzozo wa vita nchini mwake ili kuchelewesha uchaguzi mkuu.

Akihutubia viongozi wa mikoa, Tshisekedi amesema kwamba “raia wa Rwanda sio maadui wa Congo lakini utawala wa Rwanda ndio adui wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.”

Matamshi yake yameonekana kama majibizano baada ya rais wa Rwanda Paul Kagame, alipokuwa akiwahutbia wabunge wa nchi hiyo wiki iliyopita, kusema kwamba “hii shida inaweza kusuluhishwa iwapo nchi hiyo inayojitayarisha kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao, haijaribu kutengeneza hali ya dharura ili uchaguzi usifanyike.”

Kagame alisema hayo wakati alikuwa anaeleza wabunge wake kuhusu mzozo kati ya Rwanda na DRC, ambapo aliendelea kufutilia mbali ripoti kwamba Rwanda inawasaidia waasi wa M23.

“Kama anajaribu kutafuta njia nyingine ya kuahirisha uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, basi atumie sababu nyingine na sio Rwanda,” alisema Kagame bila kutaja jina la Tshisekedi.

"Raia wa Rwanda ni ndugu na dada zetu, utawala wao ndio adui wa DRC"

Tshisekedi, naye amesema kwamba “raia wa Rwanda ni ndugu na dada zetu lakini wanahitaji msaada ili wawe huru. Msiwachukulie kama maadui lakini kama ndugu zetu wanaohitaji kuungwa mkono ili kujiepusha na viongozi kama wao wanaotumia mbinu za kitambo za miaka ya 80 na 90, mbinu za vita wakati bara la Afrika tumeamua kwamba hatutaki vita.”

Hivi karibuni, Tshisekedi alitangaza usajili wa wanjeshi kadhaa ili kulinda nchi yao na pia akatangaza kuongeza bajeti ya ulinzi ya Congo.

Serikali ya Rwanda inashutumu DRC kwa kuunga mkono waasi wa FDLR na kuwashirikisha katika jeshi la nchi hiyo.

DRC nayo inshutumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23 wanaopigana mashariki mwa nchi hiyo.

Nchi zote mbili zimekanusha madai hayo.

Waasi wa M23 wamekataa kuondoka katika sehemu ambazo wamedhibithi, pamoja na kuacha vita, licha ya viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki na mjumbe wa Umoja wa Afrika kuwaamurisha kufanya hivyo.

Waasi wa M23 wanasisitiza kwamba wanapigana kulinda watu wa asili ya Kinyarwanda, wanaoishi DRC, dhidi ya mashambulizi ya makundi ya waasi likiwemo kundi la waasi la FDLR.

Mjumbe wa Jumuiya ya Afrika mashariki kwa ajili ya amani DRC Uhuru Kenyatta akizungumza katika mkutano wa wa kutafuta amani DRC, uliofanyika Nairobi, Kenya. Nov 30, 2022
Mjumbe wa Jumuiya ya Afrika mashariki kwa ajili ya amani DRC Uhuru Kenyatta akizungumza katika mkutano wa wa kutafuta amani DRC, uliofanyika Nairobi, Kenya. Nov 30, 2022

Mazungumzo ya amani yamemalizika Nairobi

Mkutano kati ya makundi ya waasi na wapatanishi wa jumuiya ya Afrika mashariki umemalizika Nairobi Jumanne bila ya makubaliano maalum namna ya kumaliza vita vya waasi mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Makubaliano pekee kwenye mazungumzo hayo ni kwamba mazungumzo zaidi yataendelea kufanyika kati ya serikali ya DRC na jamii mbali mbali zinazoishi mashariki mwa nchi hiyo

Mjumbe wa jumuiya ya Afrika mashariki, anayesimamia mazungumzo hayo, Uhuru Kenyatta, amesema kwamba mazungumzo hayo ni mwanzo wa kutafuta amani ya kudumu nchini Congo.

Kati ya maswala yaliyojadiliwa ni namna jamii zinazoishi mashariki mwa DRC zinaweza kufaidika na utajiri wa madini uliyo sehemu hiyo, na ambao umekuwa sababu kubwa ya migogoro.

Mkutano wa Nairobi utafuatiwa na mikutano mingine kadhaa ya mazungumzo kati ya rais wa DRC Felix Tshisekedi na makundi ya waasi kote nchini humo.

Kundi kuu la waasi la M23, ambalo limekuwa likipigana na wanajeshi wa serikali, halikuwa na waakilishi katika mkutano wa Nairobi.

Mapigano yamekuwa yakiendelea kati ya kundi la M23 na wanajeshi wa serikali kwa siku kadhaa sasa, licha ya pande zote kukubaliana kusitisha mapigano.

Majibizano kuhusu watu waliouawa

Serikali ya Congo imesema kwamba wapiganaji wa M23 wameua raia 270 katika mji wa Kishishe.

Umoja wa mataifa umesema kwamba umepokea ripoti za mauaji ya raia wakati wa mapigano kati ya kundi la M23 na makundi mengine ya waasi katika mji wa Kishishe.

Watu wanaokimbia vita mashariki mwa DRC, Kibumba, kaskazini mwa Goma
Watu wanaokimbia vita mashariki mwa DRC, Kibumba, kaskazini mwa Goma

Msemaji wa kundi la M23 Lawrence Kanyuka, amesefutilia mbali ripoti kwamba kundi hilo linawalenga rai ana kutaja jumuiya ya kimataifa kuchunguza kilichosababisha vifo hivyo.

Kanyuka ameshutumu wanajeshi wa serikali na makundi mengine ya waasi kwa kuashambulia kile ametaja kama ngome zao.

Amedai kwamba serikali ya DRC haitaki mazungumzo ndio maana wanajeshi wake wanaendelea kushambulia ngome za kundi la M23.

Wajumbe wa amani wa jumuiya ya Afrika mashariki wamesema kwamba jumuiya hiyo itafuatilia hatua zitakazokuwa zimepigwa kwa ajili ya amani DRC, mapema mwaka ujao.

Mkutano utakaofuata wa amzungumzo utafanyika katika miji ya Bunia na Goma, mashariki mwa Congo.

XS
SM
MD
LG