Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 19:36

Trump asema mkutano na Kim huenda usifanyike


Rais Donald Trump (kulia), Kiongozi wa Korea Kaskazini (kushoto)
Rais Donald Trump (kulia), Kiongozi wa Korea Kaskazini (kushoto)

Rais wa Marekani Donald Trump amesema mkutano wake uliopangwa kufanyika na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un huenda usifanyike mwezi ujao (Juni).

Trump alitoa tathmini yake juu ya hatua zilizofikiwa na pande mbili za Washington na Pyongyang juu ya mkutano huo, wakati alipokutana na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in huko White House.

Trump amefafanua: "Na unajua, kuna uwezekano kuwa mkutano huo utafanyika. Kuna fursa hiyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba usifanyike. Sitaki kupoteza muda mrefu na nina uhakika kuwa yeye (Kim wa Korea Kaskazini) hatapendelea kupoteza muda mwingi. Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa kwamba hautafanyika na hilo ni sawa. Hiyo haimaanishi kuwa hautafanyika – hapo baadae. Lakini inawezekana usifanyike mwezi Juni 12. Lakini kuna fursa nzuri kuwa tutafanya mkutano huo.”

Trump amesema “kuna masharti fulani tunataka iwepo na masharti hayo bila ya shaka tutayafikia.”

Trump alikataa kueleza masharti hayo, lakini alisema kuwa hilo la kuondolewa silaha za nyuklia Korea Kaskazini lazima lifanyike.”

Wakati huohuo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema Jumanne, Marekani bado inaendelea na maandalizi ya mkutano wa Juni 12.

“Mwenyekiti Kim alitaka kuwepo mkutano huu. Rais Trump alikubali kuhudhuria. Tulianza kutafuta tarehe na sehemu ya kukutana. Tumepata hizo tayari. Na kuanzia hapo, tunaendelea na maandalizi. Ni wazi kuwa – tunaendelea, tunaendelea kuhakikisha kuwa tunafikia makubaliano juu ya ajenda za kujadili katika mkutano huo. Lakini ninaendelea kuwa na matumaini,” ameeleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.

Korea Kaskazini imeeleza kuwa inaweza kusitisha mkutano kwa sababu kuna kuhitalifiana juu ya masharti yaliyotolewa na Marekani juu ya nchi hiyo kulazimishwa kuondosha silaha zake za nyuklia.

Trump amesema hadharani juu ya kumlinda Kim iwapo ataondosha silaha za nyuklia katika nchi yake, lakini mpaka sasa hakuna tamko lolote la kumjibu Trump kutoka kwa kiongozi wa Korea Kaskazini

XS
SM
MD
LG