Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 05:52

Trump anataka kura za Wisconsin kurudiwa kuhesabiwa wakati hesabu ya Georgia ikikamilika bila mabadiliko


Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa kampeni Milwaukee - Wisconsin
Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa kampeni Milwaukee - Wisconsin

Rais wa Marekani Donald Trump ameasilisha maombi ya kutaka kura katika jimbo la Wisconsin, kurudiwa kuhesabiwa.

Trump anataka kura kuhesabiwa upya katika majimbo mawili makubwa ambayo yana idadi kubwa ya wafuasi wa chama cha Democratic, akidai kwamba wizi wa kura ulifanyika katika majimbo hayo.

Hakuna Ushahidi wowote umetolewa kudhibitisha madai yake.

Amelipa dola milioni 3 zinazohitajika ili kura hizo kuhesabiwa upya.

Shughuli hiyo inatarajiwa kuanza leo alhamisi na ni lazima ikamilike kabla ya Desemba tarehe moja.

Joe Biden, alimshinda Donald Trump kwa kura 20,608 katika kaunti za Milwaukee na Dane, ambapo hesabu ya kura itarudiwa.

Kwa kawaida, shughuli ya kurudia kuhesabu ya kura kote Marekani huwa haibadilishi hesabu ya kwanza.

Trump alishinda jimbo la Wisconsin katika uchaguzi wa mwaka 2016 na chini ya kura 23,000 na kupinga ombi la kutaka hesabu ya kura irudiwe.

Kwingineko waziri wa mambo ya nje wa jimbo la Georgia Brad Raffensperger, amesema kwamba marudio ya hesabu ya kura katika jimbo la Georgia huenda yasibadilishe ushindi wa Joe Biden.

Amesema kwamba shughuli hiyo inakaribia kumalizika na kwamba kaunti chache zinasubiriwa kuasilisha matokeo.

Wakati huo huo mahakama kuu katika jimbo la Pennsylvania imesema kwmaba itakubali kesi ya rais Donald Trump ya kupinga maelfu ya kura zilizopigwa kwa njia ya posta katika kaunti ya Philadelphia ambazo hazikuwa na taarifa za mpigaji kura kwenye bahasha.

Mahakama ya chini iliamua ijumaa kutupilia mbali kesi ya maafisa wa kampeni wa Trump kutaka kura 8,329 kutojumulishwa kwenye hesabu ya kura wakidai kwamba zilikuwa za wizi.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG