Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Januari 04, 2025 Local time: 13:39

Trump amwachisha kazi HR McMaster


Generali HR McMaster.
Generali HR McMaster.

Rais wa Marekani Donald Trump, Alhamisi alimwachisha kazi mshauri wake kuhusu usalama wa kitaifa, HR McMaster, na kumteua aliyekuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, John Bolton, kuchukua pahala pake.

Kwa muda wa wiki kadhaa kabla ya kuachishwa kazi kwa McMaster, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa za Marekani waliviambia vyombo mbalimbali vya habari kwamba huenda afisa huyo angefutwa kazi na rais Trump.

Mwezi Februari mwaka huu, McMaster, alitofautiana na Trump baada ya kuuambia mkutano wa usalama wa kitaifa mjini Munich, Ujerumani, kwamba kulikuwa na ushahidi bayana ulioonyesha kuwa Russia iliingilia uchaguzi mkuu wa Marekani wa 2016.

Yamkini kauli hiyo haikumpendeza rais Trump ambaye alijibu kupitia mtandao wa Twitter kwamba McMaster hakueleza ukweli kamili.

Hatua hiyo ya Trump ililijiri wiki moja tu baada ya hatma kama hiyo kumkumba aliyekuw waziri wa mambo ya nje, Rex Tillerson, muda mfupi baada ya waziri huyo kurejea Marekani kutoka kwa ziara barani Afrika.

Trump alitangaza kuachishwa kazi kwa Tillerson kupitia ujumbe kwenye mtandao wa Twitter, na kumteua mkurugenzi wa shirika la ujasusi, CIA, kuchukua nafasi aliyoiacha Tillerson.

McMaster, mwenye umri wa miaka 55 na ambaye ni jenerali wa kijeshi mwenye miraba mitatu, aliteuliwa kama mshauri wa usalama mnamo Februari mwaka jana.

Bolton, mwenye umri wa miaka 69, amekuwa mchambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa katika kituo cha televisheni cha Fox News, ambapo mara kwa mara, amekuwa akichukua misimamo mikali hususan kuhusu Korea Kaskazini na Iran.

Balozi John Bolton
Balozi John Bolton

Aliteuliwa kama balozi wa Marekani kwenye umoja wa mataifa wakati wa utawala wa rais George W Bush.

Taarifa iliyotolewa na White House Alhamisi jioni ilisema kuwa Bolton ataanza kazi hiyo tarehe tisa mwezi Aprili.

Mapema Alhamisi, wakili wa kibinafsi wa Trump, John Dowd, ambaye aliongoza mawakili wengine wanaomtetea rais huyo kwenye sakata ya uchunguzi wa tuhuma za Russia kuingilia kati uchaguzi wa Marekani, alijiuzulu kutoka wadhifa huo.

XS
SM
MD
LG