Mgombea wa urais wa Marekani kwa chama cha Demokratik, Hillary Clinton, alimteua Seneta wa jimbo la Vieginia, Tim Kaine kama mgombea mwenza, siku ya Ijumaa.
Hayo yalijiri siku mbili tu kabla ya mkutano mkuu wa uteuzi wa mgombea urais wa chama hicho, utakaoanza siku ya Jumatatu mjini Philadelphia, jimbo la Pennsylvania.
Bi Clinton alitoa tangazo hilo kupitia ujumbe wa mtandao wa twitter.
Uteuzi huo ulikuwa umesubiriwa na vyombo vya habari vya Marekani hususan baada ya baadhi ya maafisa wa kampeni ya Clinton kuashiria siku ya Alhamisi kwamba angetangaza mgombea mwenza kabla ya siku ya Jumamosi. Kaine ni mmoja wa wale waliokuwa kwenye orodha ya mwisho ya watu ambao Clinton alikuwa anawachunguza kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.