Chama tawala nchini Tanzania - CCM - kimemteua aliyekuwa Waziri wa Ujenzi nchini humo Dr. John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
Mkutano mkuu wa chama hicho uliokutana mjini Dodoma ulimteua Magufuli kutoka miongoni mwa wagombea watatu kwa kura 2104 au asilimia 87.1 ya kura zote, Balozi Amina Salum Ali alitokea wa pili kwa kura 253 au asilimia 10.5 wakati Waziri wa Katiba katika serikali inayoondoka madarakani Asha Rose-Migiro alipata kura 59 au asilimia 2.4 ya kura zote.
John Magufuli sasa atapambana katika uchaguzi mkuu na wagombea wa upinzani au muungano wa upinzani - UKAWA - ambao wanatazamiwa kutangaza mgombea wao baadaye wiki hii.
Utaratibu wa kupata mgombea kwa chama cha CCM ulikuwa mrefu baada ya kuanza na wagombea zaidi ya 40 lakini katika siku tatu za mikutano mjini Dodoma chama hicho haraka kilipunguza wagombea hao kuwa watano - Magufuli, Amina Salum Ali, Asha Rose Migiro, Bernard Membe na January Makamba.
Katika ngazi iliyofuata Membe na Makamba waliangushwa na kubakia wagombea watatu walioingizwa katika mkutano mkuu wa wajumbe wa chama na kupigiwa kura.