Wingu la kisiasa limetanda mjini Dodoma, Tanzania wakati chama tawala nchini humo CCM kikiwa katika utaratibu wa kuteua mgombea atakayewakilisha chama hicho katika uchaguzi mkuu wa rais Octoba 25.
Ripoti za hivi karibuni zinasema Halmashauri Kuu ya chama hicho, NEC, imemaliza kikao chake ambacho kilikuwa kinajadili majina matano ya wagombea waliopitishwa na kikao cha awali cha Kamati Kuu ya chama. Vyanzo vya kuaminika vya habari vinasema NEC imejadili majini ya wagombea hao watano – Bernard Membe, Asha Rose Migiro, John Pombe Magufuli, Amina Salum Ali na January Makmaba – bila kuongeza majina yoyote mengine kama ambayo ilikuwa invumishwa.
Baadaye leo usiku, majira ya saa mbili, NEC itatangaza majina ya mwisho matatu na kuyawasilisha kwa mkutano mkuu wa chama ambayo utaanza kikao chake saa tatu usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Hali ya taharuki ilizuka kote nchini na hasa mjini Dodoma baada ya Kamati Kuu kutangaza majina matano kati ya watu 32 waliokuwa wakiwania ugombea huo.
Macho zaidi yalikuwa kwa waziri mkuu wa zamani nchini humo Edward Lowassa ambaye aliokuwa anaonekana kama anaongoza katika mbio hizo kutokana na makundi ya watu waliokuwa wakimkaribisha katika mikutano yake ya kampeni za awali kote nchini.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama walijitokeza mbele ya waandishi wa habari Ijumaa usiku na kusema kuwa hawauingi mkono maamuzi yaliyofikiwa na Kamati Kuu katika kupitisha majina hayo matano.
Wakati huo huo, mwanasiasa mmoja wa upinzani anasema mvutano ndani ya CCM utaongeza nafasi ya muungano wa upinzani kushinda uchaguzi mkuu. Tundu Lissu wa Chadema aliambia VOA kuwa muungano wa vyama vya upinzani, UKAWA, utatumia mpasuko unaojitokeza katika zoezi la kupata mgombea CCM kupata waungaji kutoka chama hicho tawala.
Alisema hivyo baada ya Kamati Kuu ya CCM kumwondoa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa kutoka kwenye orodha ya wanasiasa wanaotaka kuwania urais kupitia chama hicho.
Wapinzani wake wamekuwa wakimshutumu kwa kugawanya watu na kuhusishwa na ulaji rushwa. Lowassa anakanusha madai hayo.
Kamati Kuu ya CCM ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete anayeondoka madarakani aliondolewa katika majina matano ya wagombea wa awali iliyotangazwa Jumamosi asubuhi.
Wachambuzi wanasema kuondolewa kwa Lowassa huenda kukasababisha mpasuko katika chama hicho, na kuupa upinzani mwanya wa kushinda uchaguzi wa rais.