”Rais una nafasi ya kipekee kuweka historia ya maridhiano katika taifa letu kwani kuna wengine wanalalamika wanaumia. Rais tumia nafasi hii ukaliweke taifa katika hali ya utengamano,” amesema Mbowe.
“Nimekuja kushiriki sherehe za miaka 58 ya Uhuru kama uthibitisho wa ulazima wa kuwepo maridhiano, upendo, mshikamano katika taifa letu. Namuomba Mungu siku ya leo ikafungue milango tuweze kuishi kama taifa linalopendana, tuvumiliane, tukosoane, turuhusu demokrasia.
Ametoa ujumbe huo leo Desemba 9, 2019 katika sherehe hizo zilizofanyika kitaifa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mbowe ameshiriki katika maadhimisho hayo huku akiwa na kesi ya uchochezi mahakamani kwa zaidi ya mwaka sasa, sambamba na viongozi wenzake nane, lakini pia kukiwa na zuio la kutofanya mikutano ya hadhara.
Pia, kumekuwa na malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu kubinywa kwa demokrasia nchini, hivyo ujumbe wa Mbowe unamuomba Rais Magufuli kujenga maridhiano kati ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wapinzani.
Mbali na Mbowe, viongozi wengine wa Chadema waliohudhuria sherehe hizo ni Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu; Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na wengine.
Imetayarishwa na mwandishi wa VOA, Washington DC.