Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini Tanzania-TAKUKURU imetoa tamko la kupambana na rushwa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.
Akizungumza katika mahojiano jijini Dar Es Salaam, Jumanne Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hosea, alisema kwa sasa taasisi hiyo inawachunguza baadhi ya wagombea walionunua vifaa au vitu mbali mbali na kuvigawa kwa wananchi na iwapo wamefanya hivyo kwa kuvunja sheria ya gharama za uchaguzi na wakiridhika na ushahidi watawakamata watu hao na kuwafikisha mahakamani.
Mkurugenzi huyo amesema iwapo mgombea anataka kugawa vitu kwa wananchi anatakiwa kupeleka misaada hiyo kwenye chama chake na kisha itawafikia walengwa kwa kuwa nia ya TAKUKURU ni kuona kuwa uchaguzi mkuu unakuwa huru, wa haki na bila rushwa.
Uchaguzi nchini Tanzania unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Unavishirikisha vyama vya upinzani pamoja na chama tawala cha CCM.
Sauti ya Amerika imezungumza na Msajili wa vyama vya siasa nchini humo John Tendwa na kwanza kutaka kujua sheria hizi zinatekelezwa vipi.