Shirika moja la msaada wa kisheria linapanga kuishtaki serikali ya Zanzibar na wengine waliohusika katika uzembe uliosababisha moja ya ajali mbaya kabisa kupata kutokea katika usafiri wa majini Afrika Mashariki.
Kundi hilo lisilo la kiserikali linalotoa msaada wa kisheria - Zanzibar Legal Service Centre -linatoa wito kwa serikali kuanzisha uchunguzi huru na kuwashtaki wote waliohusika kwa janga hilo.
Mkurugenzi mtendaji wa muda Harusi Mpatani anaeleza kwamba “ tunajua kwamba kuna watu wengi ambao hawakufanya kazi zao vizuri. Ndio maana meli ilijaza kupita kiasi, kulikuwa na mizigo mingi ambayo haikutakiwa kuchukuliwa na wengine wanasema kwamba meli haikuwa katika hali nzuri ya kiufundi.”
Bibi Mpatani anasema shirika lake linashauriana na makundi mengine ili kufungua kesi pamoja. “Tunafikiria kwanza kuishtaki serikali, serikali kwa ujumla, kisha baada ya hapo wamiliki wa boti, kisha waziri wa usafirishaji, ambaye kwa mujibu wa sheria yetu anahusika na yeye ni mtu mwenye uwezo wa kuiruhusu meli kusafiri au la.”
Kamishna wa polisi Zanzibar Musa Ali Mussa ameiambia Sauti ya Amerika kwamba polisi hivi sasa wanalenga kwenye maji kati ya pwani ya Tanzania na Pemba, moja ya visiwa vitatu ambavyo vinakamilisha eneo la Zanzibar. “Tunatumia helikopta kutathmini eneo zima kutoka Tanga kuelekea Pemba ili kuangalia kama kuna miili yeyote ya watu waliokufa au walionusurika katika eneo hilo. Upepo unavuma kutoka eneo la tukio kuelekea eneo hilo-kutoka Pemba kwenda Tanga.” Kamishna Mussa ameiambia Sauti ya Amerika kwamba wachunguzi wanahitaji kujua sababu za ajali hiyo.
Bibi Mpatani anasema kesi hiyo huwenda ikawajumuisha maafisa kutoka Tanzania bara ambapo meli ilianza safari yake kutoka Dar-Es-Salaam na iliripotiwa meli kujaa tangu huko. Anasema waathirika wameliambia kundi lake kwamba kwa maneno yao “uzembe wa makusudi umefanyika” Waogeleaji wa Afrika kusini wanatafuta miili iliyokwama ndani ya mabaki ya meli.
Meli ya MV Spice Islander ilitengenezwa kubeba abiria 600. Watu walionusurika wanaripoti kuwa meli hiyo ilibeba abiria kutoka 800 hadi 1,000.
Wakati huo huo mashahidi katika mji mkuu wa Kenya wanasema dazeni ya watu wamekufa kutokana na mlipuko wa bomba la mafuta. Maafisa wa polisi mjini Nairobi wanasema miili 61 imepatikana hadi sasa, lakini wanatarajia idadi ya vifo kuongezeka. Zaidi ya waathirika 100 walioungua moto walipelekwa kwenye hospitali za eneo, baada ya bomba kulipuka Jumatatu katika eneo la watu maskini la Sinai.
Shirika moja la msaada wa kisheria linapanga kuishtaki serikali ya Zanzibar na wengine kufuatia uzembe uliosababisha ajali ya meli