Serikali ya Taliban nchini Afghanistan imethibitisha Jumapili kwamba wamewakamata raia kadhaa wa kigeni, wakiwemo Wamarekani wawili, kwa shutuma za kukiuka sheria za nchini humo.
Zabihullah Mujahid, msemaji mkuu wa Taliban ameiambia redio ya serikali ya Afghanistan kwamba wameifahamisha Marekani kuhusu kukamatwa kwa raia wake. Hakutoa maelezo zaidi, wala hakueleza uraia wa wageni wengine waliokamatwa.
Ndugu na maafisa wa Marekani wamemtambua mmoja wa Wa-marekani waliokuwa kizuizini kuwa ni Ryan Corbett, wakati utambulisho wa mtu wa pili haujatangazwa. Hii ni mara ya kwanza kwa Taliban kukiri hadharani kuwatia mbaroni raia wawili wa Marekani.
Hadi sasa, walikuwa wameripoti tu kukamatwa kwa Corbett. Alikamatwa mwezi Agosti 2022, mwaka mmoja baada ya kundi hilo la Ki-islamu kupata tena madaraka nchini Afghanistan kufuatia kuondolewa kwa wanajeshi wa nchi za magharibi walioongozwa na Marekani baada ya karibu miaka 20 ya vita, wakati huo wakijulikana waasi wa Taliban.
Forum